Bila wewe Yamoto Band haingefaulu - Beka Flavour amsifia Aslay

Msanii huyo alifurahia kurejea kwa Aslay kwenye muziki na kusema kuwa yeye ndiye alikuwa nyuma ya mafanikio yao wengine.

Muhtasari

• Karibu tena kwenye uwanja wako Mkang’afu mashabiki zako tulikukosa sana na umerudi kwa kishindo na ngoma mbili - Beka Flavour.

Beka Flavour amsifia Aslay
Beka Flavour amsifia Aslay
Image: Instagrm

Beka Flavour, msanii ambaye alikuwa mmoja wa bendi ya Yamoto na wenzake Aslay, Enock Bella na Mbosso amefurahia urejeo wa Aslay kwenye kuandika na kutunga tena mashairi ya muziki  baada ya kimya cha muda mrefu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Beka Flavour amemkaribisha Aslay, rafiki wake wa muda mrefu na kumtamkia maneno ya kheri.

Alsay baada ya kusainiwa na lebo za RockStar na Sony Music Entertainment, aliingia studioni na kuachia ngoma mbili, ya kwanza ikiwa kama kumbukumbu ya mama yake Mozzah huku ya pili ikiwa ni collabo aliyomshirikisha kamanda wa shughuli hizo, Harmonize kwa jina Follow Me.

Hizi ngoma zinakuja wiki moja tu baada ya kuachia mfululizo wa filamu hadi vipindi 5 akizungumzia maisha yake kwa jumla tangu alipoanza muziki hadi kufikia hapo alipo sasa.

Beka Flavour alimsifia na kumwambia kwamba yeye ndiye alileta ufanisi katika kundi la Yamoto na bila yeye wengine hawangemudu kufanya muziki wa biashara mpaka sasa.

Karibu tena @aslayisihaka mimi nakuita fundi wa huu mziki ndugu yangu hatujazaliwa pamoja lakini moyo wako ni wa kipekee sana, binafsi naamini bila wewe kukunjua nafsi yako na kukubali kutubeba sisi ndugu zako kwenye wimbo wetu wa kwanza uliotutambulisha kama bendi lakini kama wasanii wapya kwenye gemu hili inawezekana tungetoka lakini kwa kuchelewa kidogo, karibu tena kwenye uwanja wako Mkang’afu mashabiki zako tulikukosa sana na umerudi kwa kishindo na ngoma mbili,” Beka aliandika.

Aslay, baada ya kusambaratika kwa kundi la Yamoto, alianza kufanya kazi kama msanii wa kujitegemea ambapo alifana sana ila hapa kati akaja kupotea kabisa kiasi kwamba mashaiki zake hawakuwahi kumsikia kwa zaidi ya mwaka mzima.

Katika filamu hiyo ya Mimi ni Bongo Fleva, msanii huyo alipata kuzungumzia mengi yaliyokuwa yakiendelea nyuma ya pazia katika maisha yake huku akisema kuwa aliumia sana kumpoteza mama yake lakini pia kusongwa na mawazo, ulevi na wanawake karibia vimsafirishe jongomeo kabla siku yake kuwadia.