Mchekeshaji wa muda mrefu Eric Omondi si mgeni katika kuzua vituko na visa ndani na nje ya nchi.
Msanii huyo safari hii amepakia video akiwa na gitaa kubwa huku akiwaimbia watoto wadogo mashinani, na kusema kuwa ni safari ambayo ameanza ili kutafuta vipaji vipya mashambani.
Katika video hiyo, Omondi kama kawaida yake alizua vichekesho na utani alipowaambia watoto hao kuwa alitaka kuwaimbia wimbo wa kulia, huku akiigiza kulia.
Watoto hao zaidi ya watano ambao walikuwa wanamzingira kwa mshangao na furaha walishindwa kuzuia vicheko vyao huku Omondi akitoa sauti za kulia.
Alisema kuwa kipindi hicho cha kutafuta talanta za watoto mashinani kitaanza kupeperushwa kwenye runinga moja ya humu nchini huku akiwaahidi mashabiki na wafuasi wake kuwa itakuwa ni furaha ambayo hawafai kuikosa.
“Wimbo mpya mjini, Imekuwa Ajabu sana kuzunguka nchi nzima nikitafuta vipaji Vipya na ngeni na siwezi kusubiri nyie kuona hawa masupastaa,” Omondi aliandika kwenye Instagram yake.
Kutangaza kipindi hicho hakukuwa gumzo, bali jinsi alivyokuwa akiimba kwa kutoa sauti ya kilio na jinsi midomo yake ilivyokuwa ikijipinda na kujigeuza haswa ndicho kilivutia wengi na kushindwa kuzuia vicheko vyao.
Wengine walisema kuwa hawatangoja kusubiri ngoma hiyo na kuona jinsi alivyolia kwenye wimbo mzima kwa sababu alisema wimbo wote maudhui yake ni kulia.
“Ni wimbo ya mapenzi na huyu aliachwa na mke, inaitwa (sauti ya kulia)” Omondi aliwaambia watoto hao waliojawa na vicheko.
Kusema kwake kuwa aliamua kutafuta vipaji vipya ni njia moja ya kuendeleza vita vyake dhidi ya wasanii wa humu nchini ambao muda wote amekuwa akiwashtumu kuwa hawana ubunifu wa kutunga mashairi mazuri na pia kuwavutia mashabiki katika matamasha yao.
Omondi ndiye mwanzilishi wa kauli mbiu ya #Paly75%KE ambapo anaeneza kampeni za kutaka miziki ya kutoka nje kupigwa marufuku humu nchini huku ile ya ndani ikipewa nafasi ya hadi asilimia 75 kwenye mawimbi ya vyombo vya habari.
Mapema mwaka huu, aliwasilisha muswada bungeni kujadiliwa ili kuwa sheria kuwa muziki wa Kenya unafaa kupewa nafasi kubwa kinyume na ilivyo sasa ambapo miziki ya kigeni imetawala nchini.