Weezdom: Nilipata msongo wa mawazo nilipoondoka EMB ya Bahati Kioko

Alisema alizama katika ulevi mkali kutokana na msongo wa mawazo huku akishindwa kujikwamua kifedha.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema hata mama watoto wake walikuwa wanashindwa kumwelewa kutokana na kuona ako vizuri kwenye mitandao ya kijamii.

Msanii Weezdom,
Msanii Weezdom,
Image: Instagram

Aliyekuwa msanii chipukizi wa injili nchini Kenya Weezdom amefunguka wazi na kukiri kuwa alizama kwenye msongo wa mawazo baada ya kuvunja uhusiano wake na msanii aliyemtambulisha kwenye Sanaa ya miziki ya injili, Bahati Kioko ambaye pia alimsainisha mkataba kwenye lebo yake ya EMB.

Weezdom alisema kuwa baada ya kuzorota kwa uhusiano wake na Bahati mpaka kuonesha tofauti zao hadharani mitandaoni, alishindwa kujikimu kifedha na hivyo kuzama kwenye lindi la mawazo lililomsababishia kutafuta faraja kwa vileo ambavyo pia havikumsaidia bali kuzidisha matatizo yake.

Akizungumza katika podcast ya EMM, Weezdom alisema kuwa kuzama katika ulevi kulimpoteza kutoka njia kuu hata akajisahau kufanya muziki na kufilisika pakubwa.

“Niligundua kuwa sikuwa na budi kuruhusu mambo yawe sawa nilipokuwa na hasira. Baadaye nilipigwa na watu ninaowafahamu lakini kisa kiko mahakamani hivyo siwezi kuzungumzia sana. Nimekuwa nikiingia na kutoka hospitalini tangu Januari hadi Julai na watu wengi hawakujua. Pia nilizama katika mshuko wa moyo wakati huo na kuanza kutafuta kimbilio,” Weezdom alisema.

Msanii huyo alijipata katika skendo chafu baada ya kuanza kuchafuana mitandaoni na kumtukana aliyekuwa mpenzi wake Mylee Stacey huku akiwa pia na mwanasosholaiti Manzi wa TRM ambaye walitoa ngoma moja naye kabla ya kukosana na kuanza kutupiana cheche.

“Kulikuwa na changamoto nyingi lakini sikuwahi kushiriki na mtu yeyote hivyo niliamua tu kunywa pombe. Nilikuwa nikinywa kutoka asubuhi hadi jioni. Huu mwaka nimekua nampambana. Nilikuwa nakunywa peke yangu na kujificha ili mtu asijue kuwa nilikuwa nakunywa,” msanii huyo mpotefu alisema.

Msanii huyo alizungumza jinsi baadhi ya watu wema walijitokeza kumkamua kutoka lindi la ulevi wakiwemo watangazaji Willy Tuva na aliyekuwa mbunge wa Starehe Jaguar.