Larry Madowo alalama ugumu wa baadhi ya maneno ya Kiswahili cha Tanzania

Mwanahabari huyo wa CNN alisema kuwa Watanzania wanafaa kudhibitiwa katika kuasisi baadhi ya maneno changamano kama hayo.

Muhtasari

• Madowo alishangazwa kuwa Watanzania wanaita simu ya smartphone kwa jina na Kishkwambi.

• Alionekana kutokubaliana nao na kusema kuwa maneno hayo yanachagizwa tu.

Larry Madowo ateta ugumu wa Kiswahili cha Tanzania
Larry Madowo ateta ugumu wa Kiswahili cha Tanzania
Image: Hisani

Mwanahabari wa kimataifa wa CNN kutoka Kenya, Larry Madowo amepigwa na butwaa kutokana na ugumu wa baadhi ya maneno ya lugha ya Kiswahili ambayo Watanzania wanatumia.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, Madowo alianzisha gumzo hilo akisema kuwa alishangazwa na Watanzania kuita simu ya ‘smartphone’ kuwa ni kishkwambi.

Larry madowo alionekana kutokubaliana nao katika hilo huku akisema kuwa majirani hao wa Kenya upande wa kusini wanachagiza sana katika baadhi ya maneno ya Kiswahili sanifu.

“Watanzania huziita smartphones “vishkwambi” kwa Kiswahili sanifu. Wanatunga tu maneno sasa,” Larry alisema.

Hapo ndipo mmoja wa Watanzania alimcharukia na kumrekebisha kuwa kishkwambi si smartphone kama ambavyo alikuwa anasema balihiyo ni kompyuta ndogo aina ya tablet, huku pia akimwambia smartphone kwa Kiswahili ni simu janja.

“Hapanaa Larry 🤣 vishkwambi ni kompyuta ya tablet - simu mahiri ni simu janja!

Laptop ni tarakilishi mpakato AU kipakatalishi  pole aisee!” Maria Sarungi Tsehai alimmrekebisha.

Madowo alionekana kuchananyikiwa zaidi na kusema kuwa ni wakati sasa Watanzania wafanyiwe udhibiti dhidi ya kutunga maneno changamano kama hayo.

“Watanzania sasa wanahitaji kudhibitiwa, maneno yote ni kama yamechagizwa pakubwa kama ni kweli,” Madowo alilalama.

Kiswahili ni lugha rasmi katika Afrika Mashariki lakini wakazi wengi nchini Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini wanatatizika kujieleza katika lahaja hiyo.

Nchini Tanzania, Kiswahili kinadumisha hadhi ya lugha rasmi na ya taifa na pia kimepitishwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).