"Harmonize anakutana na wapenzi wake kwenye gym" - Idris Sultan

Harmonize walionekana na mwanadada huyo pamoja ingawa hajadhibitisha ikiwa wanachumbiana.

Muhtasari

•Harmonize hajadhibitisha ikiwa mwanadada huyo ni mpenzi wake lakini alikubali maoni ya watu kuwa wanashabihiana huku akisema amechanganyikiwa.

Harmonize asemekana kuwakuta wapenzi wake kwenye gym
Harmonize asemekana kuwakuta wapenzi wake kwenye gym
Image: Instagram

Ikiwa ni siku moja imepita tangu msanii Harmonize aonekane na mwanamke mmoja msanii ambaye kwa jinsi walivyokuwa wanadekezana kwenye picha na video, wengi walihisi kuna kitu kinachoendelea baina yao zaidi ya urafiki, watu wameanza kuzua dhana mbalimbali.

Harmonize baada ya kuonekana na mwanadada huyo ambaye alitaja jina lake kwenye chapisho lake kama Feza Kessy, Wadadisi wa mitandaoni hawakusita kuingia kwenye akaunti ya yule mwanadada na kudurusu baadhi ya picha zake, ambapo waliibuka na jibu moja kuwa, Kessy ni mpenzi wa gym kama tu mpenzi wake wa awali, mwigizaji mkongwe Fridah Kajala Masanja.

Mwigizaji Idris Sultan hakuachwa nyuma katika kueneza dhana hii ambayo kupitia Instastory yake, aliandika kauli hiyo iliyodhaniwa kuzungumzia mapenzi ya Harmonize akisema, “Huwa anawakuta kwenye gym.”

Kajala ni mpenzi wa mazoezi ya gym muda mrefu na wakiwa katika huba lao, aghalabu walikuwa wanapakia video na picha wakishiriki mazoezi kwenye gym na Harmonize.

Kwa upande mwingine, mwanadada Kessy pia alionekana kwenye gym katika baadhi ya picha zake, moja akiwa amesimama mbele ya vyuma vya gym na nyingine akiwa ndio anajishughulisha kunyanyua vyuma kufanyisha mwili zoezi.

Japo minong’omo imekuwa mingi kuhusu iwapo wanachumbiana au ni kazi tu wanafanya pamoja, Harmonize kwenye Instastory yake alisema kuwa tayari ameanza kuchanganyikiwa na kupagawa kutokana na maoni ya wengi kuwa wanapendeza na kushibana pamoja na mwanadada huyo.

“Mnanichanganya mnavyosema kuwa tunapendeza, ingawa hata sisi wenyewe tumeona hivyo,” alisema.

Tayari Harmonize ametoa nguo kwa jina ‘Wote’ ambamo mwanadada huyo ndiye ameshiriki kama vixen.