Unajifanya bikira na unalala kwa kitanda na wasichana 2 - Eric Omondi amjibu Stevo

"Ruger ana meneja mmoja anapanda ndege "first class" na wewe una mameneja 4 unapanda basi."

Muhtasari

• Siku moja iliyopita, Stevo alitoa wimbo akimuita Eric mnafiki anayejifanya anampenda kumbe ndio anamsema kinyemela.

• Eric naye ameachia wimbo akimjibu Stevo na kumkejeli kuhusu uongozi wake ambao haujui kumtetea msanii wao.

Omondi na Stevo watupiana maneno katika nyimbo
Omondi na Stevo watupiana maneno katika nyimbo
Image: Instagram

Siku moja tu baada ya msanii Stevo Simple Boy kuachia wimbo kwa jina ‘Haya Basi’ akimsuta mchekeshaji Eric Omondi kuhusu kumtaka kuwafuta mameneja wake wa muziki, mchekeshaji huyo naye ameingia studioni na kurekodi wimbo wa kumjibu Stevo vikali.

Eric Omondi na Stevo wamekuwa wakirushiana maneno tangu mwishoni mwa mwaka jana ambapo msanii huyo alidaiwa kudhulumiwa katika shoo ya So Fire Fest iliyofanyika Mombasa ambapo Eric Omondi alikuwa MC.

Baadae Omondi alitoa tamko la kutaka uongozi wa Stevo kujiuzulu kwa kumfelisha msanii wao ambaye hakutokea kwenye ukumbi kutumbuiza pamoja na msanii kutoka Nigeria, Ruger.

Omondi baada ya kukandiwa vikali na Stevo Simple Boy ambaye alimtaja kama mnafiki anayejifanya kumpenda kumbe ndio anamsema nyuma ya pazia, sasa naye amejibu vikali huku akisema kuwa msanii huyo anafaa kupigwa viboko.

“Unajifanya bikira na unalala kwa kitanda na wanawake wawili, Ruger ana meneja mmoja na anaabiri ndege kitengo cha daraja la kwanza ilhali wewe una mameneja wanne lakini unasafiri kwa basi. Nimewaandalia collabo na mnalala kwa darasa, sasa hivi mnanitafuta, nitawapiga kwa glasi. Kwanza mnafaa kupigwa na viboko. Mnakula elfu 80 na hamjalipwa,” Omondi aliimba.

Kinachoshangaza wengi ni kwamba Msururu huu wa mashambulizi kutoka pande zote mbili unakuja kwa njia ya nyimbo ambapo wasanii wote wanaonekana kama ndio mwanzo mkoko unaalika maua kwani hakuna dalili ya kupata mwafaka hivi karibuni.

Stevo kwenye wimbo wake naye alitaja kuwa Omondi na wenzake walimuita kwa shoo na hawakumlipa na kumuacha akila matumbo.

“Eti Simple kuja shoo, nitakulipa na baada ya shoo nakula matumbo huku wakileta shobo na zogo,” Msanii huyo aliimba akiuliza yule rais ndio nani – akimlenga Omondi ambaye anajiita rais wa Ucheshi Afrika