Lily Asigo, mkewe mwanamuziki JuaCali asimulia safari ya uzazi, adokeza kupata mtoto wa 4

Siwezi kungoja kuwa na mazungumzo ya watu wazima na wanangu wote - Asigo.

Muhtasari

• Mama huyo wa watoto 3 alisema kila mimba ilikuja na mafunzo yake tofauti katika maisha yake.

• Alisema katika safari ya ulezi, alifanya makosa na kujifunza kwani hakutaka kujibeba kama mwanamke shupavu.

Juacali na mkewe watarajia mtoto wa 4
Juacali na mkewe watarajia mtoto wa 4
Image: Instagram

Lily Asigo, mkewe mwanamuziki mkongwe wa genge, Jua Cali amedokeza kuwa huenda akapata mtoto wa nne pamoja na msanii huyo hivi karibuni.

Mama huyo wa watoto watatu mpaka sasa alipakia picha ya watoto wake watatu na kuibua kumbukumbu jinsi safari yake ya ulezi imekuwa tangu alipobeba ujauzito wa kwanza mpaka sasa ambapo amewalea watoto watatu na wote ni wakubwa.

Kwenye picha hiyo, Asigo aliandika ujumbe mrefu akisimulia jinsi kila mtoto alimpa fundisho la aina yake huku pia akidokeza kuwa mtoto mwingine ambaye atakuwa wa nne atakuja kwa njia yake ya kipekee kama ambavyo hawa watatu wa awali walikuja.

Kulingana na Asigo, kila mtoto alikuwa na fundisho tofauti huku akidokeza kuwa kama mama wengine tu, mtoto wa kwanza alimpata kama hakuwa anajua chochote kuhusu uzazi huku akitumia uzoefu huo kurekebisha mengi katika mtoto wa pili na wa tatu.

Alisema kuwa kuwaona wanawe wamekuwa watu wazima kunampa faraja kuwa alijitahidi kama binadamu kufanya makosa na kujirekebisha katika kile alisema kuwa haikuwa ndoto yake kuwa mama bora bali kutoa malezi bora kwa wanawe.

“Sijawa mzazi yule yule mmoja kwa watoto wangu watatu. Nikiwa na mzaliwa wangu wa kwanza, sikujua chochote kuhusu kuwa mama. Nikiwa na wa pili, nilirekebisha katika mengi; na wa tatu, nilimdekeza kama yai na kupuuza baadhi ya mambo. Hivi sasa wote wana mama ambaye anajua anachotaka, anajiamini sana, anajiruhusu kufanya makosa na asiwe mama bora. Mtoto mwingine nitakayemlea pia atakuwa tofauti. Siwezi kungoja kuwa na mazungumzo ya watu wazima nao wote,” Asigo alisema.

Ni kama mwaka huu 2023 umeanza kwa vishindo vya aina yake kwa watu kudokeza kuongeza mtoto katika familia yao kuwa miongoni mwa malengo yao makuu.

Wiki jana pia Kabi Wa Jesus pia aliodokeza kuwa mwaka huu huenda akaongeza mtoto wa tatu katika familia yake, mwaka mmoja tu baada ya kubarikiwa na mtoto wa pili – binti ambaye walitangaza ujio wake mwezi Aprili mwaka jana.