Mrembo Kinuthia: Tiktoker Kelvin Kinuthia atoboa pua na kuvaa kipini

Je, ni kweli mwanaume akitoboa maisha hatua inayofuata ni kutoboa pua?

Muhtasari

• Kinuthia anaingia kwenye chama cha wanaume waliotoboa pua kama Diamond Platnumz na Harmonize.

Kinuthia atoboa pua
Kinuthia atoboa pua
Image: Instagram

Mwanatiktoker Kelvin Kinuthia amezidi kujiongezea urembo huku akiasi jinsia yake ya kiume na kukumbatia zaidi jinsia ya kike.

Kinuthia katika ongezeko la mapambo yake ya hivi karibuni ni kutoboa pua!

Alipakia picha kwenye ukurasa wake wa Twitter akiwa ametoboa pua na kusema kuwa pambo hilo ndilo la hivi karibuni ambalo ameliongeza kwa ulimbwende wake, huku kipini hicho kikiwa kimeangaza kwelikweli puani mwake.

Kando na kutoboa pua, Kinuthia pia alifichua kuwa ameongeza kutoboa sikio lake kwa mara ya pili kama njia moja ya kuzidisha urembo na mitikasi yake mitandaoni.

“Hatimaye nilipata kutoboa pua na sikio langu kwa mara ya pili kutobolewa ️   nilisisimka sana,” mwanamitindo huyo ambaye hajawahi zungumzia hadharani hali yake ya kijinsia alisema kwa mbwembwe.

Mashabiki na wafuasi wake wengi ambao wameshamzoea na uvaaji wake walimhongera kwa kuongeza pambo hilo la puani huku wakimwambia kuwa yuko sawa, lakini pia baadhi walizidi kumsimanga kutokana na hatua yake ya kujiweka sana kike hali ya kuwa yeye ni mtoto wa kiume.

Wengine pia walitaka Kinuthia kuwaonesha jinsi mama yake alihisi alipooona mwanawe ametoboa pua.

“Hicho kipini cha puani kinakuvaa vizuri, unaonekana umeng’ara mtoto wa kike,” Jannet Audi alimwambia.

“Tuoneshe jinsi mama yako alihisi ulivyomtokea na kipini puani,” mwingine alimuuliza.

“Kuwa mwanamke ni gharama sana, ona sasa unallazimika kugharamikia vitu visivyofaa ili tu kuturidhisha sisi wanamitandao,” Jacky alimzomea.

Mwanamitindo huyo wa Tiktok amekuwa akiwaacha vinywa wazi baadhi ya watu kwenye mitandao haswa kutokana na uvaaji wake wa kike, na hivi karibuni ameanza kujitokeza wazi kabisa na kujiita mtoto wa kike licha ya kuwa menye jinsia ya kiume.

Kutoboa kwake pua kunamjumuisha kwenye orodha ya wanaume ambao wamefanya hivo katika ukanda wa Afrika ya Mashariki wakiwemo wanamuziki kutoka Tanzania, Diamond Platnumz ambaye aligonga vichwa vya habari mwaka jana alipotoboa pua akiwa nchini Malawi, na pia Harmonize ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionekana na kipini cha puani.