Huddah: Nataka mwanaume Mrusi haraka iwezekanavyo, siwezi olewa na Mwafrika

Afrika haina mustakabali angavu - Huddah Monroe.

Muhtasari

Siwezi olewa na Mwafrika kwa sababu tutaendelea kujigaragaza katika mateso yale yale ya bara la Afrika - Huddah.

Huddah Monroe aomba kupata mwanaume Mrusi
Huddah Monroe aomba kupata mwanaume Mrusi
Image: Instagram

Mwanamitindo wa muda mrefu nchini Huddah Monroe amefunguka ukweli wake kuwa hatokuja kuota akiolewa na Mwafrika huku akitoa sababu zake kuhusu hilo.

Huddah alisema kuwa kama kuna mwanaume ambaye atakubali posa yake bila kupepesa jicho wala kuangalia nyuma mara mbili mbili basi ni Mrusi.

Kulingana na Huddah, bara zima la Afrika halina musitakabali angavu na kutwa kucha ni kuhangaika na umaskini, jambo ambalo hakuumbiwa yeye.

“Mustakabali wa Afrika si angavu hata kidogo asikudanganye mtu. Nataka mwanamme wa Mrusi haraka iwezekanavyo. Siwezi olewa na Mwafrika kwa sababu tutaendelea kujigaragaza katika mateso yale yale ya bara la Afrika,” Huddah aliandika.

Huddah ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionesha chuki yake kwa nchi yake Kenya na Waafrika wote hadharani aliwahi nukuliwa akisema kuwa yeye hutumia muda mwingi nje ya nchi kama vile Dubai katika kile alisema kuwa Kenya hakuna sehemu nzuri za kujivinjari na huwa hajihisi salama akiwa nchini.

Mwanasoholaiti huyo alisema kuwa bara la Afrika muda wote ni mtumwa wa dola za Kimarekani katika kile alionekana kuchukizwa baada ya kukatwa tozo kubwa katika miamala ya baadhi ya biashara zake za bidhaa za kujipodoa.

“Hivi viwango vya ubadilishaji dola vinaniumiza, Afrika hakuna mustakabali, ni watumwa wa dola,” Huddah alilalama.

Hii si mara ya kwanza kwa Huddah kudokeza kuwa analilia ngoa suala la ndoa huku akiweka masharti makali kwa ladha ya wanaume ambao atakubali posa yao.

Aliwahi nukuliwa akisema kuwa hawezi kubali kuoleka kwa mwanaume ambaye amelelewa na mama kwani katika ndoa hiyo, watakuwa wanang’ang’ania usikivu kutoka kwa kijana huyo na mama mkwe, huku akisema endapo atakubali ndoa ya aina hiyo basi itakuwa ni kwa sharti kuwa mama mkwe awe amefariki.