Malejendari wa muziki Wyre, JuaCali na Nameless watangaza kuunda bendi ya muziki

Wyre alifichua habari hizo kupitia video aliyoipakia Twitter.

Muhtasari

• Nameless alipakia picha ya watatu hao wakiwa wamebarizi na kuwataka watu waibue kumbukumbu zao kuwahusu.

Malejendari wa Muziki Kenya kuunda bendi moja
Malejendari wa Muziki Kenya kuunda bendi moja
Image: Facebook

Msanii maarufu wa muziki kutoka nchini Kenya Wyre the love child amefichua habari mpya kwamba ameamua kuunda bendi ya wasanii wa kizazi kipya wa zamani pamoja na wenzake.

Msanii huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter alipakia video akitoa tangazo hilo lakini kwa jinsi ambavyo alianza kutoa tangazo hilo, karibu awape wengi mshtuko wa moyo.

Wyre alianza kwa kusalimia mashabiki wake kabla ya kuanza kupasua mbarika kama mtu ambaye anatoa taarifa mbaya za kufikia ukomo wa jambo fulani, lakini kwenda mwisho wa klipu hiyo, alifichua kuwa wameungana na kutengeneza timu ya malejendari wa muziki.

“Kuna nini jamani. Kwa kawaida sifanyi hivi. Imekuwa zaidi ya miaka 20 katika kufanya jambo hili la muziki na nadhani ni kuhusu wakati huu ambao umefika…. Unajua kila kitu kinafikia hatua hiyo ya kufika mwisho. Kwa hivyo nimeamua ... hii ni ngumu. Tumeamua kuwa tunaunda bendi ya wavulana wa kitambo,” mwimbaji huyo alitangaza huku akihamishia kamera kwa wasanii wengine.

Wasanii maarufu wanaojiunga na bendi hiyo ni pamoja na Nameless, Jua Cali na Kenzo.

Baadhi ya mashabiki wake walifurahia taarifa hiyo ila hawakukosa kumsuta kwa jinsi alivyowapandisha presha mwanzoni mwa video akianza kama mtu anasema habari mbaya.

“Kidogo nitoe ile hancifu nyeupe nilipewa na Muiru 2007 nipanguze machozi gosh,” Thirsty Kipsoiwet alisema.

“Wah! Mjinga sana, jinsi nilivyokuwa nikishusha pumzi! 20yrs coming... Wavulana wazee, leteni!” Winnie Njuguna alimwambia.

“Moyo wangu ulikuwa kwenye viganja vyangu..wafalme wetu wa burudani..Kama ningekuwa CS wa sanaa, tungekuwa na matembezi ya umaarufu pale KNT. ____ itazinduliwa kwanza, kisha nyinyi watu mmoja baada ya mwingine,” mwingine alisema.