MC Jessy atokea na sketi, aibua maswali mengi kuliko majibu

MC Jessy sasa anaingia kwenye orodha ya Eric Omondi na Kinuthia ambao wanavalia mavazi ya kike.

Muhtasari

• Wengi walimchamba na kutaka kujua maana ya kutokea na vazi hilo la wanawake haswa wakati huu ambapo suala la LGBTQ limeteka mawimbi nchini.

Mchekeshaji MC Jessy avalia nguo za kike
Mchekeshaji MC Jessy avalia nguo za kike
Image: INSTAGRAM,

Mchekeshaji na mwanasiasa MC Jessy amezua maswali kwenye mitandao ya kijamii baada ya kupakia picha akiwa amevalai sketi na kubeba kibegi kidogo cha wanawake.

 

Chapisho hili japo kwa maudhui yake halikuwa linahusiana kivyovyote vile na masuala ya wapenzi wa jinsia moja au wanajamii wa LGBTQ, wengi walizua maswali katika mrengo huo huku wakitaka kujua ni kwa nini ameamua kutokea kwa muonekano wa kike.

Jessy kuonekana katika mavazi ya kike kunakuja wakati ambapo nchini kuna mjadala sugu kuhusu wanachama wa LGBTQ kufuatia kifo cha mwanaharakati wa jamii hiyo Edwin Kiprotich Kiprop almaarufu Chiloba.

Jessy hakutaka kujali watu watasema nini kuhusu maswali ya LGBTQ na yeye alilificha swali lake kutaka kujua maana ya hicho kibegi kidogo ambacho haswa wanawake hukibeba kwa mbele.

“Wale mnajua sana, hiki kibegi ni cha nini?” MC Jessy aliuliza.

Wengi hawakutaka kujibu moja kwa moja bali walienda moja kwa moja kutaka kujua iwapo naye ndio mwanzo ameamua kujitangaza wazi kuwa mmoja wa mrengo ule mwingine au ni mitikasi yake ya kawaida tu mitandaoni.

“Ni vizuri kutokea kuliko kuteseka moyoni, nyinyi ni wengi,” David Mugo alimwambia.

“Wazazi wetu wa Meru wakikuona tu na huu muonekano, mwaka 2027 kama utajaribu siasa tena hii picha itaibuliwa,” Kesh Mackenna alimtahadharisha.

“Wachana na begi kwanza, hiyo sketi umevaa maana yake ni nini?” Rophy Qeenmelanin alitaka kujua.

Baadhi walionekana kumtetea dhidi ya kashfa za kuitwa mwanachama wa LGBTQ huku wakisema kuwa ni utamaduni wa baadhi ya mataifa ambapo wanaume huvalia jinsi hiyo.

“Si kila mtu anafikiria kuwa amejitokeza kama mpenzi wa jinsia moja, kama hujawahi safari kwenda mataifa ya Fiji, Scotland, Burma, huwezi elewa kuwa huu ni utamaduni tu,” The Kenyan Don alisema.

Itakumbukwa kuwa huyo si mchekeshaji wa kwanza kutokea na mwonekano wa kutiliwa mashaka kwani mwaka jana mchekeshaji Eric Omondi wakati anaigiza kipindi chake cha Divalacious, alikuwa anatokea na mavazi ya kike pamoja na kujipodoa - jambo lilizowaaminisha wengi kuwa huenda ni mwanachama wa LGBTQ japo mwenyewe alikanusha madai hayo vikali na kusema kuwa ni mitikasi yake tu alikuwa anajaribu kufanikisha.