Zuchu bado ni singo, hajamtambulisha mwanamume yeyote kwangu! - Khadija Kopa asisitiza

Kopa alisema kuwa kutokana na umaarufu wake na bintiye, siku atamtambulisha mpenzi wake dunia nzima itajua, na kusema hilo bado halijatokea.

Muhtasari

• Zuchu ni maarufu hata mimi Mama yake ni maarufu siku atakapopata Mchumba akanitambulisha matajua tu - Kopa.

Khadija Kopa, Zuchu, Diamond Platnumz.
Image: HISANI

Khadija Kopa, mamake msanii Zuchu kutoka WCB Wasafi amerejelea na kusisitiza maneno yake kuwa mwanawe bado yuko singo na hana mwanaume yeyote awe mchumba au mpenzi.

Kulingana na malkia huyo wa mipasho ya Taarab, bintiye hachumbiani na msanii Diamond kama ambavyo wengi wamekuwa wakiaminishwa kwa muda mrefu wa zaidi ya mwaka mmoja na miezi kadhaa sasa.

Kopa alisema kuwa kutokana na umaarufu wa Zuchu, siku akipata mchumba dunia nzima itajua na itakuwa ni habari ya mijini na vijijini, ila kwa sasa akawataka watu kuwa na subira na kutopotoshwa na kile ambacho wamekuwa wakikisikia mitandoani na kwenye mablogu ya udaku.

Zuchu bado yupo single, hana Mpenzi wala Mchumba na wala hajanitambulisha kwa Mwanaume yoyote kwamba Mama huyu ndiye Mwanaume wangu, Zuchu ni maarufu hata mimi Mama yake ni maarufu siku atakapopata Mchumba akanitambulisha matajua tu muwe na subira,” Khadija Kopa alisema.

Kauli hii inakinzana na kauli kutoka kwa Zuchu na msanii Diamond Platnumz ambapo mwaka jana walinukuliwa pakubwa wakidokeza kuwa huenda ni wapenzi ila hawakuwa wanataka jambo hilo kufahamika hadharani kwa watu wengi.

Itakumbukwa kwamba mwishoni mwa mwaka jana katika hafla ya uzinduzi wa albamu ya Juma Jux ‘King of Hearts’ msanii Diamond alitokea kama mgeni mwalikwa na aipata nafasi ya kuzungumza.

Kabla ya kuanza kuzungumza, Diamond alitaja ngoma ambayo alikuwa anaipenda kutoka kwa albamu hiyo ambapo alisema ni ile ambayo Jux alimshirikisha Zuchu, ya “Nidhibiti” akimtaja Zuchu kama mke wake.

“Mimi binafsi ngoma yangu pendwa kwa hii albamu ni ile ambayo Jux amemshirikisha mke wangu Zuchu,” Diamond alisema huku watu wakishangilia.

Zuchu naye katika video moja wakiwa na rafiki yake, alionesha picha ya Diamond na kuulizwa kama anamjua, na bila kusita alidamka na kusema “ndio huyo namjua ni mpenzi wangu.”

Aidha, hatua ya Diamond kumuita Zuchu kama mke wake bila hata ya dhibitisho la ndoa ilipata pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu ambao walisema msanii huyo anahitaji toba kwa kukufuru kumtaja mtu kama mke wake hali ya kuwa hawana Baraka yoyote ya nikkah.

“Umetukosea sana sisi tuliopo kwenye ndoa . Nikwambie tu NDOA SIO KWAPA. Unamuitaje Zuchu MKE WAKO ? Wakati hauja OA . Kwa sheria ya kiislaamu tayari UMERITAD inabidi USILIMU TENA UWE MUISLAMU. Kwa kuongea uongo kwenye sunnah alio itekeleza mtume wetu muhammad swalla llahu alayh wasalaam,” Mwijaku alimkoromea Diamond.