Davido na Chioma wachora tattoo za majina yao vidole vya pete

Hatua hii ya kuoneshana mapenzi inakuja miezi mitatu tu tangu fununu za kufanya harusi ya kitamaduni.

Muhtasari

Wawili hao walimpoteza mwanao mwezi Novemba alipozama kwa bwawa la kuogelea nyumbani.

Mwanamuziki wa Nigeria Davido na mkewe, Chioma Kila mmoja amechora tattoo ya mwenzake katika kidole cha pete.

Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya kuripotiwa kufunga ndoa ya kitamaduni siku chache kufuatia kifo cha mwanao Ifeanyi aliyeripotiwa kuzama kwa bwawa la kuogelea nyumbani kwao Lagos.

Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Nigeria, ni watu wa karibu tu wa familia walioruhusiwa kuhudhuria hafla ya kufanya harusi ya kitamaduni, lakini bila simu zao za rununu.

Kipindi hicho ambacho kilikuwa kigumu sana kwa wawili hao, hakuna aliyedhubutu kuzungumza mitandaoni lakini blogu moja ilisema kuwa ni kweli harusi ya kitamaduni ilifanyika nyumbani kwa kina Davido ambapo mahari ya Chioma yalitolewa kwa ukamilifu.

Picha sasa ambazo zinasambazwa mitandaoni zinaonesha wawili hao kila mmoja akiwa na jina la mwenzake katika kidole cha pete, kama njia moja ya kuhakikishiana mapenzi yasiyojua kufa hata baada ya kufiwa na mwanao wa kipekee Novemba mwaka jana.

“Harusi ya kitamaduni ambayo ina watu wachache wa familia na marafiki waliohudhuria bila kamera kuruhusiwa ilifanyika katika Nyumba ya baba yake Davido na mahari ya Chioma ililipwa kikamilifu, hii inakuja baada ya Chioma kumwambia Davido kuwa hakuna kitu kingine chochote cha kuangalia kama yeye. mtoto wa kiume anayewaunganisha hayupo tena,” mwanablogu maarufu wa Nigeria, Gist Lover's Gram aliripoti kipindi hicho.

Mwanamuziki huyo baada ya kimya cha muda, alionekana hadharani wakati wa sherehe za kufunga kombe la dunia alipotumbuiza mubashara.