Harmonize amnyakua mke wa Haji Manara na kumvisha jezi yenye jina "Konde Boy"

Baada ya kudhibitisha kuachana na Manara, mwanadada huyo alionekana nyumbani kwa Harmonize akiwa amevalia jezi yake.

Muhtasari

• Rushynah alidhibitisha kuachana na Manara wiki iliyopita na kabla vumbi la timbwiri zima halijatulia, tayari ameonekana kwa Harmonize.

Harmonize amnyanganya Manara mke
Harmonize amnyanganya Manara mke
Image: Instagram

Wakenya wanakuambia mambo yamechemka kweli kweli kama mtindi wa kiasili uliotiwa hamira!

Mapya kabisa kutoka nchini Tanzania ni kwamba msanii Harmonize amemvuta nyumbani kwake mwanadada Rushynah ambaye alikuwa mke wa pili wa aliyekuwa msemaji wa timu ya kandanda ya Yanga, Haji Sunday Manara.

Rushynah wiki jana aliweka wazi kwamba amechoka ndoa ya kuwa nyumba ndogo na kujiondoa katika uhusiano wake na Manara, miezi michache tu baada ya kukubali kuolewa kama mke wa pili.

Jumamosi mitandao ya kijamii kulikuwa hakukamili baada ya mwanadada huyo ambaye ni huru kwa sasa kuonekana akiwa nyumbani kwa Harmonize huku anajiburudisha kwa kucheza mpira wa vikapu.

Alikuwa amevalia jezi yenye jina “Konde Boy” mgongoni, jambo ambalo lilizua minong’ono mingi baadhi wakisema kuwa baada ya haji Manara kula, haina neno mdogo wake Harmonize ameamua kuondoa sahani mezani.

Rushyanah alipakia video hiyo kwenye Instastory yake akiruka na mbwembwe kama lote baada ya kufanikiwa kuuweka mpira wavuni.

Sekeseke za mitandaoni zinazidi kuchukua mikondo na mitazamo tofauti kila sekunde iendayo kwa Mungu, huku Manara na aliyekuwa mkewe wakianza kutupiana mikwara ya kutaka kuvuana nguo hadharani.

Kwa upande wake, Harmonize ambaye pia alitemwa na Kajala siku si nyingi zimepita  amejipata katika zogo hili ambapo hakutarajiwa kabisa kuvutwa kwenye jungu hilo, ila bado hajasema lolote.

Awali hadithi za mitandaoni zilikuwa zinahusisha kuvunjika kwa huba la Manara na mkewe na msanii Diamond  Platnumz ambaye picha iliibuka akimtazama Rushynah kwa macho ya kumtamani wakiwa Qatar katika kushuhudia michuano ya kombe la dunia.

Katika ziara hiyo ya Qatar, Diamond kupitia kampuni yake ya ubashiri ya Wasafi Bet ndiye alifadhili safari ya Manara na wake zake wawili na picha hiyo ilinaswa Rushyna akiwa ubavuni mwa Manara lakini ametupiana jicho na Mond.