Msihadaiwe, Ng'ang'a ni mchungaji wa kweli, maombi yake yalinikomboa - Rose Muhando

“Namshukuru Mungu kwa ajili ya baba yetu (Ng’ang’a) tafadhali wale mlioko chini ya baba huyu msiondoke miguuni pake" - Muhando.

Muhtasari

• Mwanamuziki huyo wa injili alisema aliamua kuanza mwaka kwa kupitia kanisani kwa Ng'ang'a ili kurudisha shukrani na kutoa ushuhuda wake.

• Mnamo 2019, mchungaji Ng'ang'a alionekana kweney klipu iliyosambaa akiombea Muhando huku akigaragara sakafuni.

Muhando amsifia Ng'ang'a kwa maombi yaliyomkomboa
Muhando amsifia Ng'ang'a kwa maombi yaliyomkomboa
Image: YouTube screengrab

Malkia wa nyimbo za ijnili ukanda wa Afrika Mashariki Rose Muhando amerejea katika kanisa na mchungaji Ng’ang’a kwa mara ya kwanza tangu alipokuwa pale kuondolewa mapepo miaka mitatu iliyopita.

Muhando katika ujumbe wake, alimshukuru Nga’ang’a kwa kumpa uponyaji kipindi ambacho alidai alikuwa amezingirwa na mapepo mabaya na kuwakashfu vikali wale waliosema kuwa kipindi kile alikuwa anaigiza mbele ya madhabahu ya kanisa la Neno.

“Wote mnanifahamu sina haja ya kujieleza, lakini niseme Ahsante Yesu kwa kunipa nafasi nyingine ya kukanyaga hapa kwa mara nyingine. Kipindi kile nilifika hapa kwa namna nyingine nikiwa na hali nyingine, kwa kifupi Bwana alinileta hapa ili nisaidike. Na nilisaidika,” Muhando alisema.

Alizidi kumsifia mchungaji Ng’ang’a huku akiwarai waumini wote walioko chini ya Ng’ang’a kutohadaiwa na kuondoka katika kanisa hilo.

“Namshukuru Mungu kwa ajili ya baba yetu (Ng’ang’a) tafadhali wale mlioko chini ya baba huyu msiondoke miguuni pake. Mimi naweza kuwa mfano mzuri wa wewe kutoondoka. Kwa wale ambao mliona kipindi kile nikija hapa, haya madhabahu ndiyo yaliyokuwa yameshikilia uhai wangu maana hicho ndicho shetani alikuwa anatafuta. Nilipita kote lakini bwana alinileta hapa. Nimshukuru Mungu kwa kukutumia wewe kuniombea,” Rose Muhando alisema.

Msanii huyo alisema kuwa kanisa la Neno linaloongozwa na Ng’ang’a ndilo liifanya dunia mzima ikajua ako na shida na kuanza kumfanyia maombi ya kukombolewa.

“Nani angejua niko mgonjwa aombe kama sio madhahabu haya. Hapa ndio palisababisha watu wote wakajua shida yao na kuniombea na kutoka kiti cha enzi Mungu akanikomboa,” Muhando alisema.

Klipu ya Muhando akiombea na mchungaji Ng’ang’a mwaka 2019 kilisambazwa mitandaoni akionekana anagaragara sakafuni mbele ya madhabahu huku mchungaji huyo mwenye utata akifokea kile kilichotajwa kuwa mapepo kumuachilia.

Muhando katika ushuhuda huo wake alimuomba Ng’ang’a radhi kwa kumfanya azungumziwe vibaya kipindi hicho.