Naomba radhi kwa EX wangu Anerlisa na umma kwa jumla - Ben Pol

"Nia yangu haikuwa kuumiza bali kushiriki uzoefu wangu kuhusu ndoa" - Pol.

Muhtasari

• Msamaha huu unakuja saa chache baada ya mazungumzo yanayokisiwa kuwa baina yake na Anerlisa akijaribu kumbembeleza warudiane.

Ben Pol na aliyekuwa mke wake Anerlisa Muigai
Image: HISANI

Baada ya kutupiwa maneno ya kila rangi na watu katika kile walisema kuwa anajaribu kutafuta njia ya kurudiana na mjasiriamali Anerlisa, hatimaye msanii Ben Pol ametoa taarifa ya kuomba msamaha.

Katika taarifa hiyo ambayo aliipakia Instagram yake, Ben Pol alisema kuwa anajuta kufanya mahojiano kadha wa kadha na mwanahabari Millard Ayo kuhusu ndoa yake na Anerlisa iliyovunjika huku akisema kuwa hakuwa na nia mbaya.

“Ninataka kuomba radhi kwa mambo ambayo nilisema wakati wa msururu wa mahojiano na Millard Ayo ambayo yalianza kupeperushwa January 13. Nia yangu haikuwa kuumiza bali kushiriki uzoefu wangu kuhusu ndoa, uzoefu ambao ninachukua jukumu moja kwa moja. Pia nilikuwa nataka kufunguka jinsi talaka ile iliathiri afya yangu ya akili,” Ben Pol alisema.

Licha ya kujieleza hivyo, alisema kuwa baadae alikuja kugundua kuwa maneno yake katika mahojiano yale yalikuwa yanamuumiza Muigai kitu amabcho kimemsukuma hadi mwisho wa reli na kulazimika kuomba radhi Hadharani.

“Hata hivyo, nimegundua kuwa maneno yangu yalikuwa mwiba mkali kwa Ex wangu na hivyo ninaomba msamaha kwake na kwa umma.  Hata kama ninataka kuendelea kuzungumzia kuhusu afya yangu ya akili na uzoefu wangu kuhusu hilo, nitahakikisha kwamba ninafanya hivyo kwa njia ambayo ni nzuri na yenye mwelekeo sambamba,” Ben Pol alimaliza msamaha wake.

Msamaha huu wa hadharani unajiri saa chache tu badaa ya mazungumzo yanayokisiwa kuwa baina yake na Anerlisa kuvujishwa akionekana kum bembeleza kurudiana huku katika moja ya mazungumzo hayo akimwambia kuwa mamake alikuwa anamtaka kurudi Tanzania.

Pol na Anerlisa waliachana mwaka 2021, miezi michache tu baada ya kufunga ndoa ya kanisani, jambo ambalo limekuwa likimsakama Ben katika afya yake ya akili na mpaka aliwahi weka hadharani kuwa talaka ile ilimuathiri kwa kiasi kikubwa na kumpa msongo wa mawazo.

Pia alisemekana kubadili dini kufuatia sakata hilo, japo haijawahi wekwa wazi kama ni kweli ama zilikuwa fununu tu.