Gidi ashindwa kuzuia kicheko baada ya kukutana Mzungu anayezungumza Kiswahili (Video)

"Siku hizi usisengenye wazungu hawa wengine wanaelewa hata lugha zetu za kienyeji," Gidi alisema.

Muhtasari

• “Ndio umevuka laini kama hii ni matatu. Sisi wote tumepanga laini hapa wewe unafaa urudi hapo nyuma kuna kondakta JKIA,” Mzungu huyo alisema kwa umahiri.

Mtangazaji wa redio Jambo kipindi cha asubuhi Joe Ogidi almaarufu Gidi amepakia video kwenye ukurasa wake wa Tiktok akiwa anapasua kicheko baada ya kukutana na mzungu ambaye alikuwa anazungumza Kiswahili.

Katika video hiyo, Gidi alikutana na Mzungu huyo baada ya kuvuka foleni ya kuabiri ndege bila kujua na mzungu huyo akaamua kumpa ukweli kwa lugha ya Kiswahili huku akimuuliza ni kwa nini anawaruka wengine kwenye mlolongo.

Kwa mshangao na kicheko, Gidi alitaka kujua mzungu huyo ana usuli wa eneo gani ambalo alipata kujifunza Kiswahili kwa weledi mkubwa.

“Hebu niambia ati umesema nini?” Gidi alimuuliza.

“Ndio umevuka laini kama hii ni matatu. Sisi wote tumepanga laini hapa wewe unafaa urudi hapo nyuma kuna kondakta JKIA,” alijibu huku Gidi akicheka na kumuuliza anatoka wapi ambapo mzungu huyo alimjibu, “Nimetoka hapa kwa laini na wewe rudi hapo” huku akiondoka na kumuacha mtangazaji Gidi katika mshangao na kicheko kikubwa.

Gidi alishauri wafuasi wake kwenye Tiktok kuwa alipata funzo kubwa ambalo angependa kila mtu kujifunza kuwa siku hizi hufai kuwasengenya Wazungu kwani unaweza pata unayemsengenya anaelewa kila kitu katika Kiswahili na pia lugha ya mtaani, Sheng.

“Siku niliporuka mstari wa uwanja wa ndege bila kujua basi mzungu fulani bila mpangilio akanikabili kwa kiswahili/sheng weuh😂 siku hizi usisengenye wazungu hawa wengine wanaelewa hata lugha zetu za kienyeji,” alisema.