Justina Syokau: Simtaki Ringtone sasa, namtaka Mandonga anifunze ngumi

"Hata kama nimesema 2023 sitaki kuchumbiana lakini Mandonga ni bonge la shoo" - Justina Syokau.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema baada ya Ringtone kumdhalilisha kuwa hadhi yake ni ya Vitz, sasa anamtaka Mandonga ili kumfunza ngumi.

Syokau asema anamtaka Mandonga
Syokau asema anamtaka Mandonga
Image: Instagram

Justina Syokau, msanii wa injili mwenye utata na mbwembwe nyingi ametangaza wazi kuwa sasa anamtaka mwanabondia kutoka Tanzania, Karim Mandonga.

Akizungumza na wanablogu kujibu maswali ya ndani kuhusu zawadi yake ya siku ya kuzaliwa – gari la kifahari ambalo alizawadiwa na watu ambao hajawaweka wazi, Syokau alisema kuwa sasa hataki tena kumuona msanii mwenza Ringtone ambaye alikuwa anamtamani kwa muda mrefu.

Syokau alisema kuwa Ringtone alimuonesha madharau walipokutana hivi majuzi katika mahojiano ambapo walikumbatiana lakini msanii huyo mwenye mikogo pia akamdhalilisha kwa kusema kuwa gari ambalo anaweza kumnunulia Syokau ni lile dogo aina ya Vitz tu.

Alisema sasa kutokana na kusimangwa na watu mitandaoni, anahitaji kujihami kwa weledi katika ngumi, na hivyo kumtaka Mandonga ili amfunze ngumi hizo, huku akifichua kuwa amemtungia wimbo tayari.

“Mandonga nimemuimbia wimbo kwa sababu ni staa ambaye amejitengeneze njia. Nataka kukutana naye yaani hata akiniambia leo niende Tanzania kukutana naye, sifikirii mara mbili. Mandonga nataka kukutana na wewe unifunze ngumi kwa sababu wakenya wananitukana sana. Nilifurahi kuona ameshinda pambano lile. Mandonga ninampenda na watu wanasema tunafananisha sauti, si tukutane jamani,” Justina Syokau alisema kwa mihemko ya aina yake.

Justina alizidi kuonesha kuvutiwa kwake kwa Mandonga akisema kuwa yuko singo na mwanamasumbiw huyo ni mtu mwenye afya sana ambaye amemtamani.

“Mandonga ni mtu mwenye afya hata kama nimesema 2023 sitaki kuchumbiana lakini yule ni bonge la shoo, ni mzuri sana,” Syokau alisema.

Msanii huyo mweney maneno mengi alisema kuwa wakati wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, hakutumia hata shilingi moja lakini watu walimpa zawadi mbali mbali akifichua kuwa nywele zenyewe zilimgharimu kima cha laki mbili pamoja pia na nguo nyekundu aliyotokea nayo.