Justina Syokau: Zawadi ya gari Landcruiser V8 ni ya Shilingi milioni 20

“Mtu amenipa gari, halafu unaanza kuchambua eti usukani ni mzee, wewe mwenywe hata hujashika kijiko" - Syokau.

Muhtasari

•Msanii huyo pia alisema anataka mtu ampe zawadi ya nyumba Karen ili abadilishe mazingira ya kuishi.

Syokau apewa zawadi ya V8
Syokau apewa zawadi ya V8
Image: Instagram

Mwanamuziki Justina Syokau amejibu vikali madai yanayozungushwa mitandaoni kuhusu zawadi yake ya siku ya kuzaliwa, gari la kifahari aina ya V8 Landcruiser ambalo alisema alizawadiwa.

Katika mahojiano na mwanablogu Nicholas Kioko, Syokau alisema kuwa wanaosema gari hilo ni mzee ni wale wanaomtakia mabaya huku akiwakashfu kuwa huenda hata hawajawahi kuzawadiwa kitu chochote.

“Mtu amenipa gari, halafu unaanza kuchambua eti usukani ni mzee, wewe mwenywe hata hujashika kijiko. Umepewa nini na mtu kama zawadi kwanza? Mimi nimepewa gari jipya kabisa la milioni 20,” Syokau alisema.

Wikendi iliyopita msanii huyo mwenye utata mwingi alipakia video na picha akipokezwa zawadi hiyo ya gari lakini watu wengi walionekana kutoamini kuwa ni lake bali ni kiki tu alikuwa anatafuta kwa gari la wenyewe.

Syokau amekanusha mashaka hayo akisema kuwa waliomzawadi ni familia moja kutoka Marekani huku pia akijibu ni kwa nini hakuenda na hilo gari katika nyumba yake ili kuliegesha kule.

Alisema kuwa kwake haliwezi toshea huku akitoa wito kwa mtu yeyote mwenye moyo wa kutoa kumpa zawadi ya nyumba mtaa wa Karen.

“Kiwango cha hilo gari ni Karen, kama una nyumba Karen na unataka kumpa Syokau kama zawadi tafahdali usisite, Watu wa Karen anza kunisongea,” Alisema.

Alisisitiza kuwa gari hilo ni la kwake na kuwataka wote wanaoeneza uvumi kuwa si lake kumkoma kwani mwaka wake tayari umeanza kupanuliwa kwa mafanikio na Baraka zake kama ambavyo aliimba kwenye wimbo wake.

“Lile gari limeniliza siku kama mbili sasa, naliona kila siku hata silali. Natafuta walinzi wa kulilinda ili lisiguswe na mtu. Pia natafuta dereva mashuhuri kwa sababu sitaki liwe likigongeshwa ovyo,” Justina Syokau alisema.