Hivi pia ndani unavalia 'boxer'? - Wanamitandao wamuuliza Dennis Karuri

Karuri aliwasuta watu wanaomchukia lakini bado wanaendelea kumfuatilia.

Muhtasari

• Karuri alikuwa amepakia picha nzuri akiwa amevalia nguo za kike na kujipodoa kwa njia nadhifu.

Dennis Karuri
Dennis Karuri
Image: Instagram

Msanii wa vipodozi Dennis Karuri, aliyezaliwa akiwa mwanaume lakini anafurahia kuvaa kama mwanamke kuanzia kichwani hadi miguuni amewasuta vikali watu wanaojifanya kumchuki kucha kutwa lakini wanamfuatilia kinyemela.

Mwanamitindo huyo alisema kuwa kuna watu wengi tu ambao wanamchukia hadharani lakini bado hawachoki kufuatilia mienendo yake mitandaoni na pengine hata kufurahia mitikasi yake.

Karuri alisema kuwa watu wa aina hiyo ni wengi sana miongoni mwa wafuasi wake na kusema kuwa chuki yao humpa msukumo zaidi wa kufanya jitihada za kujitambulisha pakubwa.

“Inachekesha jinsi maoni mengi ya chuki yalivyo kutoka kwa mashabiki wanaonifuata kwa utiifu mkubwa…nawapenda wote. Wakati huo huo, upendo pia ni mwingi. Sijui ni kiasi gani ujumbe wako tamu na madokezo mazuri yanamaanisha kwangu. Ninashukuru milele. Upendo, amani, baraka na furaha kwa njia yako!” Karuri aliandika.

Tamko hili la Karuri lilijiri baada ya kupakia picha zake na watu zaidi ya elfu kumi kuipitia na kuacha maoni kiadha wa kadha, wengi wakionekana kumsuta vikali kwa kuamua kujibeba kwa njia ya kike wakati yeye ni mtoto wa kiume.

“Uko vizuri lakini miguu imekusaliti, inakaa ya mwanaume,” mmoja kwa jina Peninnah alimwambia.

“Sasa na huu unadhifu wote, ndani umevaa boxer pia au? Ninauliza tu kwa ajili ya rafiki zangu, usichukie,” Mwingine alimuuliza kwa utani.

“Hii ni nini .....Sasa hutampa raha mtoto wa kike Kila siku tazama Mya” mwingine alisema.