"Nitatoa hela!" Otile Brown awaomba Watanzania wamrudishie laptop zake zilizoibiwa

Brown alisema mashine hizo zina vitu vyake muhimu sana ambavyo hataki kupoteza.

Muhtasari

•Otile Brown alitangaza kwamba alipoteza tarakilishi mbili aina ya Macbook katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

•Alitoa nambari ya WhatsApp +25428248738 ili yeyote aliye na vitu vyake vilivyoibiwa awasiliane naye kwa mipango ya kurejesha.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Mwanamuziki wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown ametoa ombi kwa mtu aliyeiba tarakilishi zake mbili nchini Tanzania kurejesha.

Siku ya Jumanne asubuhi, Otile Brown alitangaza kwamba alipoteza tarakilishi mbili aina ya Macbook katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere , jijini Dar es Salaam mnamo usiku wa Jumatatu.

"Kwa hiyo kwenye airport ya Julius Nyerere Tanzania nimeibiwa Mac/laptop mbili ila walinzi nawatoa huduma wamekataa kutusaidia ndani ya masaa matatu. Wamekataa kuangalia kwenye cctv. Wametuzungusha muda. Usiku mrefu zaidi wa maisha yangu.

Yani wanakataa kutoa huduma wakati ku trace laptop zikiwa tu hapo karibu. Tumetoa hadi report ya police ambayo ndio utaratibu ila wakakataa," Otile alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Brown alisema anaamini angeweza kurejesha tarakilishi zake ikiwa kungekuwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na maafisa wa usalama.

Akiongea kwenye video ambayo alichapisha kwenye Instastories zake, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alisema yuko tayari kumlipa yeyote ambaye ameshikilia kompyuta hizo zale za mkononi. Brown alifichua kuwa mashine hizo zina vitu vyake muhimu sana ambavyo hataki kupoteza.

"Atakayepata laptop zangu mimi nitapeana hela. Mimi ni straight, hata sio lazima tuende kwa polisi," alisema.

Aliongeza, "Huenda saa hii unatafuta soko ya kuuza, unatafuta mteja. Content zilizo humo ndani ni muhimu sana. Mimi naweza nikakupa hela ukanirejeshea laptop zangu. Utakuwa umenifanyia favour kubwa sana,"

Mwanamuziki huyo mzaliwa wa Mombasa alifichua kuwa hajapata utulivu na hakuwa ameweza kupata usingizi kufikia wakati alipokuwa akitengeneza video hiyo.

Alitoa nambari ya WhatsApp +25428248738 ili yeyote aliye na vitu vyake vilivyoibiwa awasiliane naye kwa mipango ya kurejesha.