Nyota ya Mandonga yazidi kung'aa, azawadiwa gari baada ya pambano Nairobi

"BOSI hii kwangu ni kubwa sana nilikuwa na mawazo ya kumiliki usafiri wangu lakini Leo umeweza kunikamilishia Moja Kati ya ndoto zangu" - Mandonga.

Muhtasari

• Mwanabondia huyo alikanusha madai kuwa alikuwa hajalipwa na kusema kuwa pamoja na kamati yake, walikuwa wamelipwa kikamilifu.

Mandonga apata gari
Mandonga apata gari
Image: Screengrab//Millard Ayo

Bondia kutoka Tanzania Karim Mandonga amesemekana kuzawadiwa gari na mfanyibiashara maarufu nchini humu, siku chache tu baada ya kung’ara katika pambano la ngumi jijini Nairobi.

Mandonga alikuwa anapambana na Mkenya Daniel Wanyonyi ambaye alimshinda katika raundi ya 5 kwa muondoano wa kitaalamu.

Bondia huyo mwenye kubwabwaja sana alitangaza promo ya pambano hilo tangu wiki kadhaa zilizopita huku akisema kuwa ngumi aliyokuwa amemuandalia Wanyonyi ilikuwa na asili kutoka kwa milipuko ya mabomu katika vita vya Urusi na Ukraine kwa jina Sugunyo.

Na kweli kwa maneno yake, aliweza kumchachawiza Wanyonyi na kuzidisha tantarira zake baada ya kushinda.

Mengi mazuri yamemfuata na baada ya kudaiwa kuzawadiwa gari, Mandonga kupitia Instagram yake alimshukuru mfanyibiashara huyo huku akisema kuwa kwa muda mrefu ilikuwa ni ndoto yake kupata usafiri wake binafsi, ndoto ambayo imefanikishwa baada ya pambano la Kenya – ambalo lilikuwa la ushindi wake wa kwanza nje ya nchi.

“@dicksoundmall BOSI hii kwangu ni kubwa sana nilikuwa na mawazo ya kumiliki usafiri wangu lakini Leo umeweza kunikamilishia Moja Kati ya ndoto zangu @dicksoundmall anae toa kila siku mungu nae humpa kila siku shukran kubwa sana kaka ALLAH akuzidishie zaidi boss wangu,” Mandonga alisema.

Awali kulikuwepo na taarifa kuwa mwanabondia huyo hakuwa amelipwa bali alikuwa anafanya kwa kujinoa tu lakini madai hayo yalifutiliwa mbali na promota wake ambaye alisema fedha zote alizipokea yeye na kumtaka mchekeshaji Eric Omondi kuomba radhi ndani ya siku saba kwa kudanganya kuwa Mandonga hakulipwa.

“Mimki ndio niliipokea pesa yote ninayo, na huo ni uongo. Eric Omondi tunaweza kumchukulia hatua kwa sababu anatuchafulia jina,” Promota alisema.