Maoni kinzani Andrew Kibe akiwashauri watoto wa kiume kukoma kuwasikiliza mama zao

Kulingana na Kibe, mwanamume kama unataka kufaulu maishani, koma kabisa kuchukua ushauri wa mama yako.

Muhtasari

• Pia aliwataka watoto wa kiume kukwepa mitego ya vidosho ambao watavamia mifuko yao na kuifyonza kabisa.

Andrew Kibe atoa ushauri kwa watoto wa kiume
Andrew Kibe atoa ushauri kwa watoto wa kiume
Image: Instagram

Mtangazaji ambaye aligeuka kuwa mwanablogu wa YouTube Andrew Kibe amejipata pabaya baada ya kutoa ushauri ambao wengi waliutafsri kuwa wa kupotosha kwa watoto wa kiume.

Kibe ambaye kwa muda mrefu sasa amejijengea mrengo wake na kufahamika kama mtetezi na mshauri wa watoto wa kiume, aliwashauri wanaume kuwa njia pekee ya kufaulu katika maisha ni kukataa kabisa kuwasikiliza mama zao.

Kibe alisema pia njia nyingine kando na hiyo ni kukwepa wanawake wenye tamaa za kipuuzi pindi kijana anapopata mafanikio.

“Ushauri wa pekee ambao ninaweza kuwapa, mimi sijui kuhusu biashara, sijui kitu kuhusu kuwa mfanyikazi mzuri au hata kuwekeza, sijui kitu chochote kuhusu hayo yote lakini kitu kimoja naweza nikakushauri mtoto wa kiume, kaa mbali na vidosho. Njia pekee ya kufanikiwa maishani ukisha kaa mbali na hawa wasichana, koma kabisa kumsikiliza mama yako,” Andrew Kibe alishauri.

Ushauri huu wengi walisema kuwa alianza vizuri lakini kumalizia aliharibu kila kitu.

Wengine walimsuta vikali kuwa kutofanikiwa kwake kulingana na maneno yake ni kwa sababu pengine alikoma kumsikiliza mama yake.

“Unaposema mama unamaanisha mama au mke?” mmoja alimuuliza.

“Kwa nini unatuambia tufanye kitu ambacho huwezi kufanya? Sisi tunafurahia,” mwingine alimuuliza pia.

“Kibe umeanza vizuri hapo kwa wasichana, lakini ulipofika kwa mama yangu nilimalizana na wewe kabisa,” mwingine alisema.

Hata hivyo, kuna wengine ambao walionekana kuungana naye na kusema ukweli wao kuhusu kukaribisha wanawake katika maisha yako kama mwanamume.

“Ukweli. Wanawake wote watakudanganya. Mwanamume anayeweza kudhibiti tamaa na hisia zake za ngono huwa hawezi kuzuilika. Mababu zetu walikuwa wakienda uhamishoni kwa miezi kadhaa,” Vasco Francis alisema.

“Kifee hapa nakubaliana na wewe,wanawake wameshusha wafalme..wanaume wameuza ardhi na biashara zao walizorithi juu yao...kaa mbali nao!am one yes,but just keep away!” Rocatash alimuunga mkono.

Maoni yako ni yepi?