Harmonize amezea mate uraia wa Rwanda, asema haya kuhusu Tanzania

Wadadisi wa kisheria wanahoji kuwa Tanzania huwa hairuhusu uraia pacha na hivyo msanii huyo anahitaji kuikana Tanzania ili kuwa raia wa Rwanda.

Muhtasari

• “Nahitaji kitambulisho change cha kitaifa cha Rwanda,” Harmonize aliandika kwenye Instastory yake.

• Mshawasha huu ulitokana na kupewa mapokezi ya kifalme katika taifa hilo ambalo amelitembelea kwa ziara ya kimuziki.

Harmonzie aomba uraia wa Rwanda
Harmonzie aomba uraia wa Rwanda
Image: Instagram

Msanii wa Bongo Fleva Rajab Abdul almaarufu Harmonize amegonga vichwa vya habari katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kupakia picha ya kitambulisho chake cha taifa la Rwanda licha ya kuwa Mtanzania kindakindaki.

Ikumbukwe kuwa msanii huyo kinara wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide yuko nchini Rwanda kwa ziara ya kimuziki ambapo katika msururu wa picha na video alizopakia kutoka nchini humo, alipewa mapokezi ya hadhi ya nyota tano na watu wa eneo la Nyamirambo.

Msani ambaye pia ni mshikaji wake wa karibu kutoka nchini Rwanda Bruce Melody ndiye alimpokea na kumtembeza katika ukumbi wa Kigali Arena nchini humo ambapo anatarajiwa kufanya msururu wa matumbuizo.

Sasa kilichoshangaza wengi ni baada ya msanii huyo kuanza kujitambulisha kwa jina la ‘Kijana wa Nyamirambo’ huku akisema kuwa anamezea mate sana kupata uraia wa Rwanda.

“Nahitaji kitambulisho change cha kitaifa cha Rwanda,” Harmonize aliandika kwenye Instastory yake.

Baadae kama kuna washikaji waliokwenda kwenye utaalamu na kuunda kitambulisho hicho ambacho msanii huyo alikipakia kwenye Instastory yake akionesha furaha yake huku akiuliza nani alifanikisha kufanya ufundi na ubunifu wa aina ile.

Inaarifiwa kuwa Harmonize kwa mida mrefu amekuwa akionesha mapenzi yake kwa taifa hilo jirani la Tanzania kwa kuwa ni nchi safi na yenye mandhari mazuri hivyo aliomba kuwa Anahitaji Kupewa Kitambulisho cha Taifa cha Rwanda.

Lakini kulingana na wadadisi wa kisheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taifa hilo haliruhusu au kukubali uraia pacha na hivyo Harmonize ana moja tu la kufanya kati ya kukana uraia wa Tanzania na kuenda zake Rwanda au kubakia kuwa raia wa Tanzania na kukoma kutaka uraia wa Rwanda.