Rayvanny ajitapa kumwaga zaidi ya Ksh 2M kwa mavazi ya washiriki wa video 'Nitongoze'

Msanii huyo alisema kuwa washiriki walikuwa zaidi ya 200 ambapo kila mmoja alihitaji suti ya 200K za Tanzania, sawa na Ksh 10K.

Muhtasari

• Msanii huyo alichapisha mazungumzo yake na muongozaji wa video Ivan akimpa maelezo kuhusu vile alitaka video hiyo iwe.

Rayvanny ajigamba kwa suti za washiriki wa video yake
Rayvanny ajigamba kwa suti za washiriki wa video yake
Image: Instagram

Mkurugenzi mkuu wa lebo ya muziki ya Next Level, Rayvanny ameweka wazi jinsi alivyoratibu bajeti ya kufanya video ya goma lake jipya la Nitongoze akimshirikisha Diamond Platnumz.

Rayvanny alipakia mazungumzo kwenye Instagram yake akielezea jinsi walishirikiana na muongozaji wake Ivan kufanikisha video hiyo ambayo imetajwa kugharimu kiasi kikubwa cha pesa.

Alisema kuwa alitoa ombi kwa muongozaji wa video Ivan kwamba alikuwa anahitaji watu zaidi ya mia mbili kushirikishwa, huku wote wakiwa katika suti maalum kwa ajili ya video hiyo – kama ilivyoonekana pia kwenye video yenyewe.

Ivan alimwambia kuwa watu hao 200 kupatikana wala si tatizo lakini akamwambia kizingiti kikubwa kilichokuwa mbele yake ni kwamba kila mmoja alikuwa anataka kuvishwa suti ya thamani ya laki 2 pesa za Tanzania ili kushiriki katika video hiyo.

Kwa mshangao mkubwa kwa Ivan, Rayvanny alikubali kwa haraka kuwa angegharamia suti zote mradi tu video iwe ya haiba iliyotukuka.

Kwa hesabu za haraka, suti 200 kila moja ikigharimu laki mbili ni sawa na shilingi milioni 40 pesa za Tanzania. Takrima hiyo ukiibadilisha katika hela za benki kuu ya Kenya zinakuja zaidi ya milioni mbili.

Video hiyo ilitoka Jumapili iliyopita na awali Diamond ambaye alishirikishwa alimsifia kwa njia ya kipekee Rayvanny kwa kutokuwa bahili katika kumwaga pesa ili kufanikisha video ambayo aliitaja kama ya kimataifa.

“#Nitongoze Video ya Rayvanny akimshirikisha Simba ishatoka sasa…Kaitizame kwenye bio ya @rayvanny … Hela umewekeza kwenye Video Chui, Ninajihisi fahari kuwa katika mradi huu wako kaka,” Diamond alisema.