Sidechic aelekea mahakamani kutaka 'sugar daddy' kumnunulia gari baada ya kumuacha

mwanadada huyo alitaka mzee huyo kumnunulia gari, kumkodishia nyumba nzuri, kumpa mtaji wa biashara na kumlipa posho kila mwezi.

Muhtasari

• Mwanadada huyo alisema mzee alimpata akifanya kosi ya NYS na kumtaka asitafute kazi kwani angemfaa kwa kila hitaji.

• Mzee huyo alimkabidhi gari, akamkodishia nyumba na kuanza kumpa posho kila mwezi huku pia akimuahidi kumvisha pete.

• Baadae mapenzi yaliisha, mzee wa watu akachukua vitu vyake na kumuacha binti wa watu hoi bin taabani.

Mwanadada amtaka sugar daddy kumnunulia gari
Mwanadada amtaka sugar daddy kumnunulia gari
Image: Facebook

Mwanamke wa Ghana, Deborah Seyram Adablah, ameingia kwenye vichwa vya habari baada ya kupeleka kesi mahakamani akimshtaki mpenzi wake wa zamani kumtimizia mahitaji yake yote ambayo alimuahidi kipindi wako katika uhusiano.

Kulingana na blogu ya Ghana Celebrities siku ya Jumanne, Adablah alitaka mahakama imshrutishe ‘mpenzi’ huyo wake wa zamani ambaye ni mzee kumliko (sugar daddy) kumtimizia ahadi zote ambazo alimfanyia kipindi anamtongoza mpaka kumweka chini ya himaya yake kama mpenzi wake wa kando.

Mwanadada huyo ambaye aliuza aibu kwa wapita njia, alisema kuwa mzee huyo alimtoroka baada ya kufaidi ubuyu kutoka kwake kwa muda mrefu bila kumtimizia ahadi zote alizompa.

Katika hati aliyowasilisha mahakamani, mwanadada huyo alitaka mzee huyo kutimiza ahadi zake kwake; yaani kumnunulia gari, kumkodishia nyumba iliyoko katika sehemu ya kifahari, kumlipa posho ya kila mwezi na kumpatia mtaji wa biashara yake.

Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama Kuu mjini Accra.

Iliripotiwa kuwa Adablah alianza uhusiano na sugar daddy wakati akiwa katika huduma ya kitaifa NYS. Alimpangishia nyumba, akampa gari na alikuwa akimlipa posho ya kila mwezi ya Ghc 3,000, sawa na shilingi elfu 30 pesa za Kenya.

“Alisema alimshawishi kutochukua fursa ya ajira baada ya utumishi wake wa kitaifa kumalizika kwa ahadi ya kupata mtaji wa kuanzisha biashara. Pia alimuahidi ‘pete’ mara tu atakapoachana na mkewe,” blogu hiyo iliripoti.

Walakini, uhusiano wao uliharibika na akaondoa gari, akaacha kumlipa kodi na posho. Mpenzi pia alikataa ahadi ya kutoa mtaji kwa biashara yake na suala la kumvisha pete likawa tena basi.