Harmonize awaomba Wanyarwanda kumsamehe Diamond kwa kuahirisha shoo ya Desemba

Mwishoni mwa mwaka jana Diamond alipanga kufanya shoo kwa jina 'One People Concert' nchini Rwanda lakini akaifutilia mbali dakika za mwisho.

Muhtasari

• "Nataka kuwasihi Wanyarwanda wote wamsamehe. Najua awamu ijayo atakuja,” Harmonize alisema

Harmonzie, Diamond Platnumz
Harmonzie, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Msanii Harmonize kwa mara nyingine tena amelivuta jina la aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz mdomoni mwake akiwa katika ziara ya kimuziki nchini Rwanda.

Msanii huyo safari hii alimtaja Diamond kwa kebehi kuhusu tamasha lake la mwishoni mwa mwaka jana nchini Rwanda ambalo liliahirishwa hadi tarehe isiyojulikana.

Katika mahojiano ambayo alifanyiwa na kituo kimoja cha televisheni cha RTV, msanii huyo alikuwa anajibu kwa lugha ya Kiingereza japo alikuwa anaulizwa kwa Kiswahili.

Mwishoni mwa mahojiano hayo, Harmonize alimkatisha mtangazaji baada ya kumuaga na kusema kuwa alikuwa na jambo la kuzungumzia kabla ya kuagwa.

Hapo ndipo alipasua mbarika kuhusu shoo ya Diamond iliyofeli na kumuombea msamaha kwa niaba ya Watanzania wote kwa kile alisema kuwa katika maisha mtu huwezi jua ni nini kilitokea mpaka kuahirisha tamasha hilo, na hivyo wasimhukumu kwa kufeli kutokea.

“Pia nataka kusema hili kabla sijaondoka. Kaka yangu alipaswa kuwa na shoo wiki chache zilizopita hapa Rwanda lakini hakutokea. Sijui tatizo lilikuwa nini lakini nataka kuchukua fursa hii kwa niaba ya Watanzania wote kuwaombe mmsamehe kwa sababu najua katika maisha huwezi kujua kinachotokea. Nataka kuwasihi Wanyarwanda wote wamsamehe. Najua awamu ijayo atakuja,” Harmonize alisema huku akisisitiza kuwa lengo ni kuupeleka mziki wa Afrika Mashariki katika hatua za mbele.

Diamond kabla hajapakia kipande cha video akiwa kwenye kitanda cha hospitali mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa amewaahidi Wanyarwanda bonge la shoo ya kukata na shoka iliyopewa jina One People Concert lakini katika hatua za mwisho akaisitiza kwa kusema kuwa uongozi wake haukurishishwa na maandalizi miongoni pia mwa masuala mengine ya kiafya upande wake.