Nicah the Queen: Emma Jalamo ulinitumia 200K na nilizirudisha, achana na mimi!

Msanii huyo wa injili alisema msanii wa Ohangla amekuwa akimtongoza hadi kumnunulia tikiti ya ndege kwenda Malaysia.

Muhtasari

• Alisema kuwa mchumba wake DJ Slahver alimtoroka na watoto wakiwa Mombasa baada ya Jalamo kutokea na kumpa hundi tupu.

Nicha the Queen amtahadharisha Emma Jalamo.
Nicha the Queen amtahadharisha Emma Jalamo.
Image: Instagram

Mwimbaji wa Injili Nicah The Queen ameibua mapya kuhusu msanii wa Ohangla Emma Jalamo kumtongoza kwa kumtumia pesa nyingi na kupakia picha zake mitandaoni licha ya kujua wazi kuwa anachumbiana na DJ Slahver.

Katika ujumbe mrefu ambao msanii huyo alichapisha Instagram yake akishirikisha pia picha ya ukurasa wa Jalamo ambapo picha yake imepakiwa, Nicah alisema kuwa hatua yake kumtongoza hadharani inadhoofisha uhusiano wake na mchumba wake wa sasa.

“Najua hii itakuwa mbaya kwangu lakini sitaki kupoteza uhusiano wangu @emmajalamo tafadhali tafadhali niko kwenye uhusiano wa dhati na unaniletea shida na mtu wangu! Ulianza na simu saa za ajabu usiku sasa umezidi kuniweka kwenye Facebook...” Nicah alilalamika katika sehemu ya ujumbe huo mrefu.

Alisema kuwa msanii Jalamo amefikia hatua mbaya kabisa ya hadi kumtumia pesa nyingi kwenye MPesa pamoja pia na kumnunulia tikiti ya ndege kwenda nchi za mbali ili kujivinjari naye.

“Juzi ulinitumia 200k kwenye M-PESA yangu na kusababisha mtu wangu afikirie kuwa kuna kitu kinaendelea! Nilikurudishia pesa na ikiwa haitoshi ukaona machapisho yangu kwenye Instagram na ukanifuata Mombasa ukinipa tikiti za kwenda Malaysia na hundi tupu! Tafadhali mimi si mwanasosholaiti au mchimba dhahabu kukubali matoleo kama haya,” Nicah alilalamika vikali.

 Alidokeza kuwa jambo hilo limekwamisha uhusiano wake na Slahver ambaye alimtoroka na kumuacha Mombasa akiwa na watoto wake kwa kuhisi kuwa yeye na Jalamo walikuwa wanamchezea shere nyuma ya pazia.

Alituma ujumbe kwa mchumba huyo wake aliyemvisha pete mwishoni mwa mwaka jana kurudi kwani hakuna kinachoendelea kati yake na Jalamo.

“Nilikuambia kuwa nimechumbiwa na ulichokuwa ukisema kuwa haujali…Slahver alinitoka mimi na watoto Mombasa na mpaka sasa sijamuona! @slahverdon ukiona hii...tafadhali rudi! Kweli simjui Emma Jalamo, simjui! Umenizuia kila mahali siwezi kukufikia! Picha ulizoziona ni mpangilio ambao mtu alizipiga nilipokuwa nikimuonya….Sina chochote kinachoendelea naye!”

Watu wengi walionekana kutoamini hili huku wakisema kuwa Nicah ni mtu wa sarakasi.