Otile Brown kufanya ngoma kuhusu wazazi wanaosukuma majukumu yao kwa watoto

"Wazazi kuweni wangwana kwa watoto wenu, mambo si rahisi huku nje," - Brown alisema.

Muhtasari

• Wazazi wengi wa Kiafrika wana imani kwamba unapomaliza kumsomesha mtoto, basi moja kwa moja mtoto huyo anageuka kuwa kitega uchumi chako.

Otile Brown kuwazomea wazazi wanaowategemea watoto wao
Otile Brown kuwazomea wazazi wanaowategemea watoto wao
Image: Instagram

Msanii Otile Brown amedokeza kuwa anaendelea kuandaa wimbo wa maudhui ya kuwatupia neno wazazi ambao huwatoza watoto wao ushuru kwa kimombo Black Tax

Ushuru huu ni jukumu ambalo watoto wa Kiafrika kwa muda mrefu wamekuwa wakitwikwa na wazazi wao. Wazazi wengi wa Kiafrika wana dhana vichwani mwao kuwa pindi unapomaliza kumuelimisha mtoto, basi ni jukumu lake kukushughulikia wewe kama mzazi na kusghulikia watu wengine katika ukoo mzima.

Msanii huyo fundi wa kutunga mashairi alisema wimbo huo utakuwa hadithi ya kweli kutoka kwa mmoja wa marafiki zake ambaye alimhadithia jinsi mzazi wake amekuwa akimhangaisha.

Aliwataka wazazi kuwa wangwana kwa watoto wao kwani mambo si rahisi huku nje ambako watoto wao wanatafuta riziki.

“Nafanya ngoma kuhusu ushuru wa wazazi kwa waotot #blacktax. Maudhui haya yamehimizwa na hadhithi ya mmoja wa rafiki zangu. Wazazi kuweni wangwani kwa watoto wenu, mambo si rahisi huku nje,” Otile Brown alisema kwa sehemu.

Msanii huyo aliweka wazi kuwa shinikizo la baadhi ya wazazi kutaka kushughulikiwa na watoto wao kisa waliwashughulikia kupata elimu ndilo linasababisha watoto kupata msongo wa mawazo, unyongovu na wengine kufika pabaya zaidi na kuingiwa na fikira za kujitoa uhai.

Otile Brown alisema kuwa mwaka huu Mungu akimjaaliwa hizo ndio baadhi ya mada ambazo atazizungumzia kwa undani kupitia mashairi yake ili kuelimisha jamii na haswa wazazi kukoma kuwapa watoto presha ya kutaka kurudisha mkono kwao kisa walijitoa kuwaona wameelimika.

“Shinikizo kama hizo kutoka kwa baadhi yenu wazazi ndio husababisha msongo wa mawazo kwa watoto, na maamuzi mabaya maishani mwao. Wazazi wanaojihisi wanastahili. Mada kama hizi nitazigusia kwa sana mwaka huu inshaallah,” Otile alisema.