Awinja Nyamwalo 'Jacky Vike' afurahia kupata kazi ya ubalozi serikalini

Mwigizaji huyo aliteuliwa kama balozi katika wizara ya afya kutoa hamasisho kuhusu magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika.

Muhtasari

• Ilikuwa ni heshima kubwa kupata jukumu hili siku ile ile tunapoadhimisha siku ya dunia kwa NTDs. Tuanze kazi Sasa - Awinja alisema.

Mwigizaji Awinja akizinduliwa kama balozi wa wizara ya afya
Mwigizaji Awinja akizinduliwa kama balozi wa wizara ya afya
Image: Facebook

Mchekeshaji Awinja Nyamwalo almaarufu Jacky Vike ni mtu mwenye furaha baada ya kupata kazi ya ubalozi katika serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na rais William Ruto.

Awinja alipakia video kwenye mitandao yake ya kijamii na kufichua kwamba hatimaye ametambuliwa kama balozi wa kutoa hamasisho kwa jamii kuhusu madhara ya Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa.

Awinja alionesha furaha hiyo na kusema kuwa imekuwa ni ndoto yake siku moja kufanya kazi na wizara ya Afya nchini ili kutoa tahadhari kuhusu magonjwa mbali mbali ambayo yanawasumbua watu na yanaweza kuzuiliwa kwa njia nyepesi tu.

“Mabibi na Mabwana nawapa Balozi mpya wa Magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika (NTDs) Ilikuwa ni heshima kubwa kupata jukumu hili siku ile ile tunapoadhimisha siku ya dunia kwa NTDs. Tuanze kazi Sasa😁. Asante Wizara ya Afya - KENYA AIHD Kenya kwa fursa ya kuhudumia jamii,” Awinja aliandika.

Awinja alizinduliwa rasmi Januari 30, siku ambayo duniani kote watu wanaadhimisha siku hiyo ya kutoa hamasisho kuhusu magonjwa ya kitropiki ambayo yalisahaulika kwamba yamekwisha lakini ndio yanaendelea kuwasumbua watu kinyemela.

Kupitia Instagram yake, Awinja alishiriki video fupi inayoonyesha jinsi alivyosherehekea hafla ya Siku ya NTD Duniani iliyoandaliwa katika hoteli ya Acacia Premier mjini Kisumu.

Mwigizaji huyo wa zamani wa kipidni cha Papa Shirandula aliandamana na baadhi ya waigizaji wenza katika kipindi hicho kwenda Kisumu ambapo walitoa hamasisho kuhusu magonjwa ya NTD.