Wakati Ohangla inakutana na Mugithi...

Samidoh anamshirikisha Prince Indah kwenye wimbo huo ambao unatoka Ijumaa majira ya jioni.

Muhtasari

• Indah alipakia bango la kutangaza wimbo huo wao mpya ambao utaporomoshwa rasmi Ijumaa na kudokeza kuwa utakwenda kwa jina ‘Bado Nakupenda’

Samidoh na Prince Indah kuachia video yao Ijumaa.
Samidoh na Prince Indah kuachia video yao Ijumaa.
Image: Instagram

Msanii wa Ohangla Prince Indah amewatangazia mashabiki zake kuwa Ijumaa ya Februari 3 atatoa ngoma ya nguvu akishirikishwa na msanii wa Mugithi Samidoh.

Indah alipakia bango la kutangaza wimbo huo wao mpya ambao utaporomoshwa rasmi Ijumaa na kudokeza kuwa utakwenda kwa jina ‘Bado Nakupenda’

Wimbo huo utakuwa kwenye majukwa ya mitandao ya Samidoh huku Indah akisema kuwa ndio mara ya kwanza msanii wa Kijaluo kutoka ukanda wa Ziwa Victoria anakutana studioni na kuandika wimbo na mwenzake kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

“Tuko katika mwaka wa ahadi na ni lazima tuuanze kwa kasi ya juu. Kama ilivyoahidiwa, tuko tayari kutoa. Mto huo unatiririka kutoka mlimani hadi ziwani kwa mwendo wa kasi sana. Je, uko tayari kwa gurgling?” Indah aliuliza mashabiki wake.

Prince Indah amekuwa akifanya vizuri zaidi kimuziki, jambo ambalo liemzolea umaarufu mkubwa si tu miongoni mwa Wajaluo bali kote nchini kutokana na sauti yake nzuri.

Msanii huyo nje ya Ohangla ameshirikiana na msanii Bahati kufanya ngoma mbili ambazo zote zimefanya vizuri ajabu.

Wimbo wa kwanza ulitoka mwaka jana kwa jina Adhiambo na ulifanya vizuri sana, kwenye video Bahati na Indah waliwashirikisha waheshimiwa Babu Owino na Jalang’o.

Wimbo wa pili kwa jina Abebo ulitoka mwishoni mwa mwaka jana na ambao pia umefanay vizuri sana mpaka kumjulisha Indah nje ya jamii ya Luo.

Kwa upande wake Samidoh, amekuwa akitamba na nyimbo kali za Mugithi ambazo zinashabikiwa na wengi kwenye kumbi za starehe ndani na nje ya jiji la Nairobi.

Ujio wa wawili hao pamoja kufanya kazi ulifananishwa na wengi na handshake iliyotokea baina ya rais Kenyatta na Odinga mwaka 2018.

Ohangla ni midundo ya muziki ambayo aghalabu huitambulisha jamii ya Wajaluo katika fani hiyo huku Mugithi ikiitambulisha jamii ya Wakikuyu kutoka Mlima Kenya.