Waziri wa masuala ya vijana, spoti na talanta Ababu Namwamba ameorodhesha majina ya Wakenya maarufu nchini ambao wamejinafasi katika kazi serikalini kwenye kitengo kipya cha Talanta Hela ambacho kilibuiwa hivi karibuni.
Katika tangazo lililochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali siku ya Ijumaa Februari 10, wakenya maarufu kweney miandao ya kijamii waliramba dili hilo nono na hadhi yao kubadilika ghafla na kuwa wafanyikazi wa serikali ya rais William Ruto.
Baadhi ya walioteuliwa katika baraza hilo la Talanta Hela ni mwanablogu na ambaye alikuwa mstari wa mbele kumpigia rais Ruto kampeni za mitandaoni, Dennis Itumbi ambaye ndiye atakayeongoza baraza hilo.
Jukumu kuu ya baraza hilo litakuwa ni kukuza vipaji nchini haswa talanta za kushiriki katika michezo mbalimbali pamoja na uigizaji.
Mchekeshaji mkongwe Daniel Ndambuki almaarufu Churchill aliteuliwa pamoja na mtangazaji mpenzi wa spoti Carol Radull kuongoza vitengo vya ubunifu na spoti mtawalia.
Katika kitengo cha spoti kitakachoongozwa na Radull, atakuwa anafanya kazi na wengine kama mchezaji mstaafu wa Harambee Stars Boniface Ambani, bingwa wa zamani wa dunia wa kurusha mkuki Julius Yego na mchezaji mstaafu wa kandanda na msimamizi Sammy Shollei.
Katika kitengo cha ubunifu wa uigizaji chini na Churchill, atashirikiana na wasanii maarufu kama Jimmi Gathu na Catherine Kamau (Kate Actress), wanamuziki Esther Akoth (Akothee) na Wahu Kagwi pamoja na TikToker Azziad Nasenya.
Kamati ya wabunifu itawajibika, miongoni mwa majukumu mengine, kukusanya na kusambaza mirabaha kwa wabunifu wote, kupendekeza mifumo ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Uchumi wa Ubunifu, kusimamia Tuzo za Kitaifa za Ubunifu (Grammys za Kenya) na kuanzisha mfumo thabiti wa kuchuma mapato kwa sekta ya ubunifu, kupanua fursa za ajira na kusaidia ukuaji wa uchumi wa Kenya.