Ndio mimi ni mtoto wa mama, ni mtu pekee aliyesimama nami muda wote - Prezzo

Msanii huyo alikumbuka jinsi marafiki walimpotezea wakati ndoa yake iliingia matatizo.

Muhtasari

• Prezzo alisema mama yake ndiye mtu pekee aliyebaki naye muda wote huku akijitangaza kuwa mtoto wa mama.

Prezzo akubali yeye ni mtoto wa mama
Prezzo akubali yeye ni mtoto wa mama
Image: Instagram

Msanii mkongwe wa kizazi kipya nchini Kenya Jackson Makini almaarufu Prezzo amekiri kuwa yeye ni mtoto wa mama kwa kile alikitaja kuwa mamake ndiye mtu wa pekee aliyesimama naye kipindi kila mtu alimtenga.

Prezzo ambaye alitamba miaka kadhaa iliyopita na kibao ‘Mafans’ alisema kwamba wakati ndoa yake ilivunjika, hakuna rafiki hata mmoja alijitokeza kumpa shavu na alibaki akijiliza na kujituliza mwenyewe kando na mama yake pekee.

“Mama yangu amekuwa karibu yangu muda wote. Amekuwa name katika hali zote – mbaya na nzuri. Nimemweka mama yangu katika nyakati ngumu sana lakini ndiye mtu wa pekee ambaye muda wote ananipa shavu. Na anafanya mzaha akisema hakuna hospitali au jela siijui mimi, jambo ambalo ni kweli,” Prezzo alisema.

Msanii huyo alifunguka kwa mapana jinsi ndoa yake yenye hadhi ya kiwango cha nyota tano ilisambaratika licha ya kutumia kiasi kikubwa cha hela kuitia nakshi.

Prezzo alikumbuka jinsi alitumia takriban milioni 5 pesa za Kenya kuwafurahisha marafiki ambao hawakuchangisha hata senti kwa ajili ya harusi hiyo. Lakini tofuati zilipoibuka katika ndoa yake, hakuna hata rafiki mmoja kutoka kwa wale mamia aliowafurahisha kwa vyakula na vinywaji ghali, alijitokeza kujaribu kuwasaida kupata Amani.

“Nilitumia shilingi milioni 4.7 kufurahisha marafiki kwa ajili ya harusi yangu. Lakini hata kipindi matatizo yalitokea baina yangu na aliyekuwa mpenzi wangu, hakuna aliyekuja kutupa ushauri."

"Kati ya wale marafiki niliowaalika pale, walikula, wakanywa na kucheza, walicheka na kila kitu lakini unaona wakati ndoa yangu ilikuwa inagonga mwamba, hakuna hata mmoja wao aliyekuja kwangu kujaribu kurekebisha mambo na ninamaanisha mwisho wa siku ndivyo marafiki walivyo,” Prezzo alilalama kwa uchungu mwingi katika sauti yake.