Jose Chameleone aomba msamaha kwa kupigana busu na kaka yake Weasel jukwaani

Chameleone akiwa jukwaani na kaka yake Weasel wakati wa tamasha la Gwanga Mujje, walikulana denda.

Muhtasari

• Aliwekewa shinikizo na wanamitandao ambao walihisi wasanii hao walikuwa wanaeneza vitendo vya LGBTQ.

• Chameleone alijutia kitendo hicho na kusema kwamba mashabiki wake wengi hawakukifurahia na hivyo anajuta.

Chameleone akiwa jukwaani ambapo alibusiana na kaka yake Weasel.
Chameleone akiwa jukwaani ambapo alibusiana na kaka yake Weasel.
Image: Maktaba

Msanii wa muda mrefu wa miziki ya kizazi kipya kutoka nchini Uganda, Jose Chameleone hatimaye amenywea na kuomba msamaha kutokana na video iliyomuonesha akikulana denda na kaka yake Weasel jukwaani.

Wikendi iliyopita, msanii huyo alikuwa na tamasha lake kubwa Zaidi ambalo amelipigia debe kwa muda mrefu kwa jina Gwanga Mujje.

Tamasha hilo lilitarajiwa kufanyika tarehe 10 Februari lakini siku hiyo, mvua ya kimbunga ilinyesha na kuharibu jukwaa ambalo lilikuwa limejengwa kwa ajili ya shoo yake.

Chameleone alilazimika kulihairisha tamasha lake hadi Februari 24 na wakati wa kufanyika kwake, msanii huyo alipanda kwenye jukwaa akiandamana na ndugu yake ambaye pia ni msanii Weasel.

Wawili hao walionekana wakiimba na kupigana mabusu moto moto, jambo ambalo lilizua mvutano mkali wa hisia kutoka kwa wanamitandao ambao walihisi wasanii hao walikuwa wanatumia tamasha lao kueneza ajenda za jamii ya wapenzi wa jinsia moja LGBTQ, gumzo ambalo limekuwa likishika moto katika maitaifa mengi ya Afrika.

Chameleone alipewa makataa ya kuomba msamaha na baadhi ya makundi ambao waliapa kumchukulia hatua kali, ikizingatiwa pia nchini Uganda serikali imeweka wazi kutolifumbia jicho suala lolote la LGBTQ.

Msanii huyo alipakia video kwenye ukurasa wake wa Twitter akiomba msamaha kwa kitendo hicho huku akiahidi kuwa hakitotokea tena.

"Pole zangu za dhati kwa umma kwa ujumla" nashukuru @Mukulaa kwa ushauri na ufadhili wako - Kwa Mungu na nchi yangu. Ningependa kuwashukuru mashabiki wote waliohudhuria lakini pia ningependa kuomba msamaha kwa kitendo ambacho mimi na Weasel tulikifanya kwenye jukwaa. Najua marafiki wangu wengi hawakufurahishwa na kitendo kile. Kwa kweli ninaomba msamaha na kweli kabisa ninajutia. Pia ninaomba radhi kwa niaba ya ndugu yangu Weasel,” Chameleone alisema.