Chipukeezy: Kwa nini sanaa ya ucheshi imeenda chini Kenya

Alisema Marekani, alijifunza mengi kuhusu ucheshi wa jukwaani, jinsi ambavyo unafanywa tofauti na huku Kenya.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo alirejea nchini mwaka jana baada ya kukaa Marekani kwa muda mrefu alikoenda kufanya msururu wa shoo za ucheshi.

Chipukeezy, mcheshi wa muda mrefu.
Chipukeezy, mcheshi wa muda mrefu.
Image: Screengrab.

Wakati makundi ya watu mbali mbali wanatoa maoni na hisia zao kuhusu kutokua kwa Sanaa ya ucheshi nchini, msanii Chipukeezy anahisi tofuati.

Kulingana na mcheshi huyo ambaye kwa muda hajaonekana akishiriki katika ucheshi, Sanaa hiyo humu nchini inazidi kudidimia kutokana na watu haswa mashabiki kutokubali kazi ya wasanii wa ucheshi.

Chipukeezy ambaye amekuwa akionekana kufanya kazi kwa ukaribu na serikali ya William Ruto kama MC katika sherehe mbalimbali alisema kwamba wacheshi wengi wanajitahidi kufanya ucheshi lakini Wakenya hawaoni kama ni ucheshi, kwani wengi wamezoeana kubaini ucheshi kutoka kwa pembe ya sarakasi na vitimbi.

“Ucheshi ni kitu chenye nguvu sana, lakini watu kwa kawaida huwa hawatoi sapoti yao. Ukiweka kitu kizuri hakuna mtu anatilia maanani, watu wanataka sarakasi. Ndio maana Sanaa ya ucheshi nchini haikui. Kuna watu wengi sana, watoto wadogo unaona wanataka kuchekesha watu lakini unaona mtu hasimulii kama ambavyo unatamani asimulie…” Chipukeezy alisema.

Mchekeshaji huyo alirejea nchini mwaka jana baada ya kukaa Marekani kwa muda mrefu alikoenda kufanya msururu wa shoo na alisema kile alichojifunza kutoka kwa ucheshi wa jukwaani nchini Marekani na jinsi unatofautiana na hapa Kenya.

“Nilienda Marekani na nikagundua kwamba kila kitu ambacho ninanua kuhusu ucheshi wa jukwaani, ni bure. Nilienda nikiwa na matini ambayo nimejipanga nayo lakini huko nilipata wale wako katika dunia tofauti. Nikianza kuwapa hadithi zangu na mama hawatanielewa…” Chipukeezy alitolea mfano.