Eddy Kenzo kushirikiana na Wanyama, Olunga kufanya kazi za kijamii nchini Kenya

Msanii huyo alisema shuleni alipata ufadhili kupitia soka.

Muhtasari

• Ndio nina mpango wa kuingia kwenye ushirika na Wanyama na Olunga na tunatarajia kufanya mengi hivi karibuni, subirini. - Kenzo.

Eddy Kenzo kufanya kazi na Wanyama, Olunga.
Eddy Kenzo kufanya kazi na Wanyama, Olunga.
Image: Instagram, Goal

Msanii Eddy Kenzo ambaye mwezi jana alishiriki kwenye tuzo za muziki kubwa Zaidi duniani, Grammy amefichua kwamba ana miradi mingi ya kijamii ambayo ameratibu kufanya na wanaspoti wa Kenya.

Kenzo ambaye alikuwa anazungumza baada ya kufika nchini Kenya aliweka wazi kwamba ameratibu kushirikiana na wanasoka nahodha wa zamani wa Harambee Stars Victor Wanyama na nahodha wa sasa Michael Olunga kufanya miradi ya kuinua jamii kispoti.

Kenzo ambaye alipata ufadhili wa masomo yake shuleni kupitia talanta ya kucheza kandanda alisema kwamba licha ya kuchepuka kidogo kwenda kwa muziki na kuacha soka, bado ana mpango mkubwa sana wa kujikita kispoti kwa njia nyingine tofauti, kando na kucheza.

“Ndio nina mpango wa kuingia kwenye ushirika na Wanyama na Olunga na tunatarajia kufanya mengi hivi karibuni, subirini. Shuleni mimi nilipata ufadhili kupitia soka na sasa huwa nacheza tu kujifurahisha, kufanya mazoezi na kupunguza uzito wa mwili,” Kenzo alisema.

Mwishoni mwa mwaka jana, Kenzo alitangazwa kuwania tuzo maridadi za Grammy katika kipengele cha Best Global Music Performance, ngoma yake ikiwa ni Give Me Love aliyomshirikisha msanii Matt B.

Japo hakuibuka mshindi katika tuzo hizo zilizofanyika mwezi jana, Kenzo alifurahi kwa kuteuliwa tu kuwania, kwani hata hiyo ni hatua kubwa ambayo ilimfanya kuandikisha historia kuwa msanii wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuteuliwa kushiriki kwenye tuzo hizo.

Alizungumzia alichojifunza kutoka kuhudhuria tuzo hizo, akisema kwamba wasanii wengi wa Kiafrika wanafaa kutia bidi sana kimuziki.

“Nilichojifunza kutoka kwa Grammy ni sisi kama Waafrika tunafaa kufanya bidi sana ili kuwa na tuzo kubwa kama zile. Na kama hatutaweza kuwa wenyeji basi nasi tushiriki na tushinde kabisa, na hili litafanikiwa kama tutashirikiana nao kwa collabo,” Kenzo alisema.

Kenzo alifichua albamu yake itatoka chini ya miezi miwili ijayo na kutaja kuwa ngoma zake zitakuwa na collabo za kimataifa.

Alitaja kuwa miongoni mwa wasanii ambao ameshirikiana nao kwenye albamu hiyo ni kundi la miziki ya Reggae kutoka Jamaica - Morgan Heritage.