Arrow Bwoy afichua Iyanii kuondoka kwenye lebo yake ya Utembe World

Arrow Bwoy alimsaini Iyanii miaka michache iliyopita kama msanii katika lebo yake ya Utembe World.

Muhtasari

• Hata hivyo, Bwoy alisisitiza kuwa uhusiano wake na Iyanii bado uko mzuri kwani wanafanya kazi ya kumsambazia kazi zake.

Iyanii aondoka kwenye lebo ya Arrow Bwoy.
Iyanii aondoka kwenye lebo ya Arrow Bwoy.
Image: Instagram

Arrow Bwoy, msanii ambaye miaka michache iliyopita alianzisha lebo ya muziki kwa jina Utembe World na kumsaini msanii Iyanii, amefichua kwamba msanii huyo sasa hayuko chini ya uongozi wa lebo hiyo.

Iaynii ambaye alivuma sana kwa kishindo cha wimbo wa ‘Pombe’ alisainiwa na Utembe World lakini kwa siku kadhaa zilizopita, hajaonekana akiwa karibu na Arrow Bwoy au hata kushiriki baadhi ya kazi zake kama ilivyokuwa hapo awali.

Hali ni hivyo pia kwa upande wa Arrow Bwoy ambaye hajaonekana na Iyanii, jambo amablo lilisababisha wengi kuuliza maswali iwapo wawili hao bado wanafanya kazi pamoja kama bosi na msanii wake.

Hatimaye Arrow Bwoy amefunguka ukweli wote kuhusu Iyanii, akisema kwamba alishaondoka japo kazi zake bado Utembe World ndio inazisambaza.

“Katika maisha wakati mwingine ukiwa unasaidia mtu na akose kuonesha dalili ya kushukuru. Iyanii mkataba wake kabla hapo nilikuwa nashughulikia kila kitu kuanzia kuuza, video na kusambaza lakini baadaye mkataba tulibadilisha kutokana na ombi lake alikuwa pia anataka kujisimamia mambo mengine,” Arrow Bwoy alimwaga ubuyu.

Alisema kuwa bado wanafanya kazi na yeye kwa usambazaji wa kazi zake, kwa kuwa bado kuna pesa nyingi walikuwa wameshawekeza kwake.

“Kuna vitu tulikuwa tumekubaliana naye kwa kuwa kuna pesa tulikuwa tumemwekezea na hiyo asilimia yetu tunaipata kutoka kwa kumsambazia kazi zake, ili pia naye apate kujisimamia kabisa. Mimi sina ubaya naye na ndio maana niligeuza mkataba nikamruhusu kujisimamia,” Arrow Bwoy alisisitiza.