Georgina Njenga awasuta wanaomhukumu kwa kutoka nje kujiburudisha

Alisema kuwa kwa miezi mitatu hakuondoka chumbani kwake hata kuenda dukani.

Muhtasari

•Alisema kuwa kwa miezi mitatu hakuondoka chumbani kwake hata kuenda dukani ila tu alipoenda kliniki.

•Aliwahimiza walio kwenye hali kama yake kutokubalia mtu yeyote kuwafanya wahisi vibaya kwa kuishi maisha yao.

Mpenzi wake aliyekuwa mwigizaji wa machachari Tyler Mbaya almaarufu Bahati,  Georgina Njenga amewasuta wanaomhukumu kwa kuenda kujiburudisha.

Siku za hivi majuzi baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakimkosoa mama huyo wa mtoto mmoja kwa kuenda katika maeneo ya burudani bila binti yake mdogo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Georgina aliweka wazi kwamba licha ya kuwa na jina mama, wana majukumu mengine mengi ya kufanya akidai kuwa miezi ya kwanza ya tatu baada ya kujifungua alihisi ni kama alijifanyisha kazi kupita kiasi. Alisema hakuwa na kijakazi kwa sababu hakutaka kuleta picha ya kuwa mama mvivu na kwamba alikuwa na hofu ya kumkabidhi mwanawe kwa mtu mwingine .

Njenga aliongezea kuwa hakutoka chumbani kwake kwa miezi mitatu, labda tu alipokuwa akienda kwenye kliniki pekee. Alisimulia kuwa  alikumbwa na msongo wa mawazo na alihisi amejipoteza na wakati mwingine alilia sana na hata kumlaumu bure baba ya mwanawe, Baha, ambaye alikuwa anamsihi kujipa muda kutembea ili abaki na mtoto lakini alikataa kwa kuwa akilini mwake alihisi kuwa alihitaji kuwepo wakati wote kwa ajili yake.

Georgina alishangaa kwa nini anaulizwa maswali akitoka nyumbani siku moja ilhali kwa siku sita amekuwa ndani bila kuondoka.

"Ulimwacha wapi mtoto wako? kana kwamba nilimuacha kwa barabara au kwa wageni,  nilimuacha mahali salama na watu ambao mimi ninawaamini."

Njenga alilalamika ni kwanini baba ya mtoto wake haulizwi maswali anapotoka nje kujiburudisha na marafiki, aliongeza kuwa yeye ni mwanadada katika miaka yake ya ishirini ambaye anajaribu kutimiza ndoto zake hivo atatumia kila nafasi anayoipata.

Aliwahimiza walio kwenye hali kama yake kutokubalia mtu yeyote kuwafanya wahisi vibaya kwa kuishi maisha yao.