VDJ Jones afurahi baba yake kuhudhuria shoo yake Kisumu, "baraka za mzazi"

"Baba yangu aliamua kuja kuniunga mkono na kuona ninachofanya vizuri zaidi kwenye mashine ya DJ"

Muhtasari

• "Asante kwa wote ambao wananiunga mkono.. nyie ni DHAHABU,” Jones

Jones akiwa na baba yake kwenye klabu
Jones akiwa na baba yake kwenye klabu
Image: Instagram

Mcheza santuri maarufu nchini VDJ Jones ni mtu mwenye furaha baada ya kupata Baraka za mzazi wake wa kiume katika kazi yake kama DJ.

Jones wikendi iliyopita alikuwa na shoo ya aina yake jijini Kisumu ambapo ghafla baba yake alitokea na kuwa mmoja wa watu waliojitokeza kuhudhuria tamasha hilo.

DJ huyo alifurahia na kupiga picha na baba yake akisema kuwa ujio wake kwenye shoo yake ni ishara kuwba sana iliyomuonesha kwamba baba ametia alama ya ndio kwenye kazi ya mwanawe.

“Imekuwa wikendi iliyojaa shughuli. Lakini kwangu hii ilikuwa ya aina yake..Baba yangu aliamua kuja kuniunga mkono na kuona ninachofanya vizuri zaidi kwenye deki. Hakuna kingine unachoweza kumwomba Mungu zaidi ya maisha marefu na afya njema kwa wapendwa wako Asante kwa wote ambao wananiunga mkono.. nyie ni DHAHABU,” Jones alisema kwenye picha hiyo akiwa na baba yake.

Kwa kawaida, wazazi wengi wa Kiafrika huchukulia kazi za Sanaa kama ulaghai na utoro kwa waotot wake, na wazazi wengi huwa hawapendi kuona watoto wao wakikumbatia kazi kama hizo, wengi wakiwa na dhana kwamba mtoto ambaye atakuwa wa maana katika familia na jamii kwa jumla ni yule anayezingatia masomo na pengine kupata kazi yenye taaluma iliyotambulika kwenye maofisi mengi.

Mashabiki wa Jones walifurahia kitendo cha baba yake kumuunga mkono katika kazi ya DJ wakisema kwamba wazazi kama hao ni adimu sana kupatikana.

“Mapenzi ya baba siku zote hayawezi linganishwa na thamani ya kitu kingine chochote. Kupata mzazi ambaye anasapoti kazi yako ya sanaa ni baraka isiyo na thamani bana,” mmoja alisema.

“Haya ndio mapenzi ya Kigenje,” mwingine alisema.