Eldoret: Shabiki wa Man U atembea uchi baada ya kichapo cha Liverpool

Jumapili, shabiki huyo sugu alikuwa ameahidi kabla ya mechi kwamba Liverpool wangeichapa United, angetembea uchi.

Muhtasari

•Shabiki huyo alionekana uji akikatiza kwenye mitaa ya Eldioret akiwa na filimbi mdomoni.

Shabiki wa United, Gogo Small.
Shabiki wa United, Gogo Small.
Image: Facebook

Gogo Small, mchekeshaji kutoka mjini Eldoret ambaye pia ni Shabiki wa Manchester United alilazimika kutembea nusu uchi katika mitaa ya mji wa Eldoret, nchini Kenya, baada ya hapo awali kuweka nadhiri ya kufanya hivyo ikiwa timu yake itashindwa na Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Mchekeshaji huyo maarufu kwa jina la ‘Gogo Small’ alizua hisia kali kwa mashabiki wake baada ya kuvua nguo na kutembea nusu uchi mjini hapa baada ya kushinikizwa na mashabiki wake kutimiza ahadi yake.

Shabiki huyo shupavu wa Manchester United alivalia jezi nyeupe ya klabu hiyo kabla ya kuvua nusu uchi.

Alivaa nepi na filimbi na kutembea katika mji wa Eldoret mchana mapema Jumatatu baada ya Man U kunyukwa mabao 7 kwa nunge na Liverpool mnamo Jumapili.

Mcheshi huyo alikuwa ameahidi kwenye kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii kwamba angetembea uchi ikiwa klabu yake anayoipenda zaidi ya kandanda itashindwa dhidi ya Liverpool kwenye mechi iliyochezwa Anfield.

“Ulifikiri sitafanya hivyo . . . Nilikuwa nimewaahidi mashabiki wangu kwamba tukishindwa nitavua nguo,” mcheshi huyo anasema kwenye video hiyo iliyosambaa mitandaoni iliyochapishwa kwenye ukurasa wake.

“Iwapo Manchester (United) itashindwa naahidi kwamba nitatembea uchi kesho. Mahali ni Silverline,” lilisoma chapisho lake la awali.

Uamuzi wake uliibua hisia tofauti miongoni mwa mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

“Umetimiza ahadi yako kaka…umefanikiwa kunipata kama mmoja wa mashabiki wako waaminifu,” aliandika Mtrourist Sonko Kalunges, mtumiaji wa Facebook.