• Visjhy amekuwa bila mpenzi tangu kuachana na Stevo SImple Boy mwaka jana.
Mwanablogu wa YouTube Pritty Vishy amefunguka kwamba tangu aanze kuongeza uzuri na urembo, wanaume wengi wamekuwa wakimtupia mistari kwenye DM za kurasa zake mitandaoni.
Mwanadada huyo kutoka mtaa duni wa Kibera sasa ameamua kutoa ujumbe wa wazi kwa wanaume hao ambao wanafurika kwenye faragha zake akisema kwamba kikubwa anachokiangalia ili kukubali mtu wa kutoka naye kimapenzi basi ni pesa.
Vishy alisema kwamba mwanamume yeyote atakayemkaribisha kwenye maisha yake ni yule atakayekuwa tayari kuchukua majukumu ya kusimamia bili zake zote ambazo kwa sasa anajigharamia mwenyewe bila mpenzi.
“Kwa wanaume wote ambao wako kila mahali wakijaribu kunitongoza, notisi ya kipoole tu ni kwamba wakati unajaribu kuja kwangu kunitongoza, hakikisha unajua kwamba unakuja kusimamia bili zangu na kufanya Zaidi ya kile ninachokifanya kwa sababu sina nia ya kurudi nyuma,” Vishy alisema.
Mrembo huyo alisisitiza kwamba anahitaji mwanamume ambaye atakuwa na uelewa wa kiwango cha juu kuhusu thamani yake na kujitoa kwa hali na mali kuigharamikia thamani hiyo.
“Nahitaji mwanamume ambaye ataelewa thamani yangu. Kwa hiyo kama uko tayari kuafikia vigezo hivyo vyote basi tunaweza chumbiana,” Vishy aliongeza.
Hivi majuzi, mwanadada huyo aliradidi maneno yake kwamba hana haja na aliyekuwa mpenzi wake Stevo Simple Boy akikanusha maneno ya baadhi ya watu kwamba anamkosa sana msanii huyo wa Freshi Barida.