"Watoto ni baraka" Willy Paul akiri upendo kwa binti yake na mwanadada Mrusi

Willy Paul alimtambua Sonia kama baraka na kujivunia jinsi amekuwa mkubwa.

Muhtasari

•Willy Paul alichapisha picha nzuri ya mtoto huyo wake mwenye umri wa miaka minne na kumtaja kama Mzungu Mwafrika.

•Wiki chache zilizopita, msanii huyo alikiri upendo wake kwa binti yake na mzazi mwenzake Viktoria Shcheglova.

Willy Paul na binti yake Sonia
Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Mwimbaji wa nyimbo za mapenzi, Willy Paul kwa mara nyingine amekiri upendo wake mkubwa kwa binti yake, Sonya Wilsovna.

Siku ya Jumatano, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili ambaye kwa jina halisi ni Wilson Radido alichapisha picha nzuri ya mtoto huyo wake mwenye umri wa miaka minne na kumtaja kama Mzungu Mwafrika.

Willy Paul alimtambua Sonia kama baraka na kujivunia jinsi amekuwa mkubwa.

"Watoto ni baraka, nampenda msichana wangu sana. Sonya wangu anakua kwa kasi.... ❤️ 😍 Mzungu Mwafrika," alisema.

Takriban wiki tatu zilizopita, mwanamuziki huyo alikiri upendo wake kwa binti yake na mzazi mwenzake Viktoria Shcheglova.

Willy Paul alichapisha picha ya wawili hao na kueleza jinsi anavyojivunia maendeleo ya binti huyo wake mrembo.

"Mtazame binti yangu Sonya, amekuwa mkubwa! Muda haungojei mtu walahi. Nawapenda hawa binadamu wawili," alisema chini ya picha hizo.

Mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi kwenye taaluma yake ya takriban mwongo mmoja alihoji ni nini alichofanya ili kustahili familia nzuri kama hiyo. Pia aliahidi kuendelea kuachia muziki zaidi.

Mwaka wa 2021, Willy Paul alibainisha upendo wake mkubwa kwa familia hiyo yake na kuahidi kumshughulikia bintiye kwa hali na mali.

"Binti yangu Sonya na mama yake wanatulia tu. Kama baba, nitafanya kila kitu kumlinda binti yangu" Willy Paul aliandika video ya Mama Sonya akiwa amemshika binti huyo wao huku wakisikiliza wimbo wake 'My Woman.

Mwimbaji huyo alitangaza kuzaliwa kwa binti yake, Sonya na mwanamitindo huyo wa Kirusi mwishoni mwa mwaka 2020.

Sonya ni mtoto wa pili wa  Willy Paul ambaye anajulikana.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa kawaida huficha mahusiano yake ana mtoto mwingine, King Damian Radido Opondo ambaye alipata na mwanadada wa hapa nchini anayemtambulisha tu kama Mama Damian.