Pastor Ng'ang'a: Nimefikisha miaka 70, gitaa langu ni la thamani ya Ksh 992K, kama gari!

Ng'ang'a alisema ana magitaa 4 lakini hilo la kwanza lenye thamani kubwa alilinunua Marekani kutokana na upendo wake kwa muziki.

Muhtasari

• “Nina miaka 70, ahsante kwa neema ya Mungu juu yangu, napenda kuimba miziki ya injili - Ng'ang'a.

Mchungaji Ng'ang'a
Mchungaji Ng'ang'a
Image: Screengrab

Mchungaji wa kanisa na Neno Evangelism jijini Nairobi, Nabii James Ng’ang’a  anasherehekea kufikisha miaka 70 ambayo ameitaja kama miaka ya furaha.

Ng’ang’a ambaye kwa mara kadhaa amekuwa akitoa ushuhuda kwamba aliwahi fungwa jela mara kwa mara tangia miaka ya 1970s hadi mapema miaka ya 1990s amejisherehekea kwa ujumbe mtamu.

Alisema kwamba siri ya kuonekana mchanga licha ya umri huo mkubwa ni kwa sababu alifanya yale ambayo alistahili kufanya na kumuachia Mungu kufanya mengine.

Mchungaji huyo aidha alifichua kwamba alipoamua kuokoka, aliupenda muziki na injili na ndio maana akanunua gitaa lake la kwanza kwa karibia shilingi milioni moja.

“Nina miaka 70, ahsante kwa neema ya Mungu juu yangu, mimi ni mchungaji na pia ni mwinjilisti, napenda kuimba miziki ya injili. Nina magitaa manne, lile la gharama kubwa Zaidi nililinunua Marekani kwa takribani dola za Kimarekani 7700 (sawa na shilingi 992,000 pesa za Kenya).  Hiyo inamaanisha ni kama gari la matatu, ni ishara kuonesha jinsi ninaupenda muziki,” Ng’ang’a alisema.

Ng’ang’a pia alitetea staili yake ya kucheza densi akisema kwamba siku zote huwa hataki kujilinganisha na mtu mwingine bali ni kujiongeza Zaidi katika uzoefu na kumuimbia Mungu.

“Sijaribu kucheza bora kuliko mtu mwingine yeyote. Ninajaribu tu kucheza vizuri kuliko mimi. Kila siku huleta nafasi kwako kuvuta pumzi, vua viatu vyako na kucheza,” Ng’ang’a alisema.

“Miaka 70 ya furaha, niliamua kufanya kadri ya uwezo wangu na mengine kumuachia Mungu,” aliongeza.

Mchungaji huyo katika ushuhuda wake, alisema kwamba alipoondoka Jela, alijipata Pwani ya Kenya ambapo alianza biashara kama mchuuzi mdogo wa matunda akitumia Mkokoteni kabla ya kuyatembelea makanisa mbali mbali kujijenga kama mtumishi wa Bwana.