Eric Omondi amtoa jela machinga aliyekamatwa na 'kanju' kwa kupiga kelele akiita wateja

Mwanamke huyo alikuwa anachuuza vitu vidogo vidogo jijini Nairobi akiita wateja kabla ya Kanju kumtia nguvini na kumpeleka kituoni.

Muhtasari

• Joyce Naserian alikuwa ameandikwa kazi ya kuuza vitu vya kampuni jijini Nairobi kwa kuchuuza.

• Alipokuwa kazini akiita wateja kwa sauti, polisi wa kaunti maarufu 'kanju' walimshika na kumpeleka kituoni.

• Kituoni Central alitakiwa kulipa elfu 5 lakini zikakosa na kupelekwa mahakamani akapewa dhamana ya elfu 10 ambazo pia zilikosekana.

Eric Omondi amtoa jela machinga aliyekamatwa na kanju
Eric Omondi amtoa jela machinga aliyekamatwa na kanju
Image: Instagram

Eric Omondi hatimaye amefanikiwa katika kumtoa jela mwanadada aliyeshikwa na polisi kwa kaunti ya Nairobi almaarufu ‘kanju’ kwa kosa la kupiga kelele akiita wateja jijini.

Hadithi ya kutia huruma ya mwanadada huyo ilisambaa siku chache zilizopita ambapo alionekana akisimulia kwamba alikuwa anafanya biashara ya uchuuzi katikati mwa jiji na kipindi anawaita wateja kwa sauti, kanju wakamshika na kumtia ndani.

“Nilikuwa nje nikiita wateja na kanju walikuja wakanishika, wakanipeleka kituo cha Central na ile pesa nilikuwa naitishwa kama dhamana taslimu sikupata kwa huo wakati. Kituoni niliitishwa elfu 5 lakini nilipokosa nilipelekwa kortini nikapewa dhamani ya pesa taslimu elfu 10 ambazo pia zilikosekana,” mwanadada huyo alielezea katika video moja.

Baada ya kukosa taslimu ya dhamana, alipelekwa katika jela ya wanawake Lang’ata ambako amekuwa akikaa bila kupatiwa dhamana tena.

Mwanadada huyo alikuwa akifanya kazi ya umachinga ambayo malipo yake ni kwa ada ya mauzo.

Baada ya simulizi yake kusambaa, watu mbalimbali walijitoa kwa udi na ambary kumpa msaada, ikiwemo kumtoa jela na kumtafutia kazi nzuri ya kujikimu kimaisha.

Wahisani hao waliongozwa na mchekeshaji Eric Omondi ambaye Jumatatu mchana alipakia video akiwa katika jela ya wanawake ya Lang’ata ambapo alimtoa mwanadada huyo na kusema tayari kuna wengine ambao wamemuahidi kazi ya kufanya.

“Mpaka sasa watu wengi wamejitokeza kumpa msaada...Asante @bernicesaroni kwa kumpatia kazi. Tumemwachilia Joyce Naserian kutoka Gereza la Wanawake la Langata. Alitakiwa kukaa jela miezi 3 kwa kosa dogo na kulipa faini ya Ksh 10,000 pekee sasa anaweza kurudi kwa Watoto wake,” Omondi alisema.