Nilipofika Mbinguni nilikuta watu wote ni weupe wanafanana Wachina - Mchungaji asimulia

Alisema amemuona Yesu mara nyingi kwani yeye huenda Mbinguni mara kwa mara kushiriki mikutano ya Mungu.

Muhtasari

• Alijiwa na mwangwi mkubwa wa jua usiku akiwa amelala, akaamrishwa kupanda mgongoni mwa Simba.

• Walifanya ziara ya kuzimuni na Simba huyo, akapitishwa kwenye sehemu nyingi kama mtalii.

Mfalme Zumaridi, mchungaji maarufu wa Tanzania.
Mfalme Zumaridi, mchungaji maarufu wa Tanzania.
Image: Instagram

Mfalme Zumaridi, mchungaji wa kike kutoka mkoani Mwanza nchini Tanzania mwenye ufuasi mkubwa amefunguka kuhusu kauli zake tata ikiwemo kuonana uso kwa uso na Mungu, kwenda jehanamu na pia mbinguni kwa nyakati tofuti.

Katika mahojiano ya kipekee na mtangazaji Millard Ayo, Zumaridi, ambaye jina lake halisi ni Diana Bundala alisimulia kwamba mara ya kwanza alitokea na Mungu akiwa darasa la tatu.

“Nikiwa darasa la tatu, nilitokewa na Mungu Kwa umbo la jua, lilikuja jua ndani tumelala na mama usiku. Likamulika ndani pote pakawa na mwanga, likaanza kusema na mimi ‘mimi ni Mungu’ mara tatu. Jua hilo lilikuwa linachezacheza kwenye ukuta likiwa na sauti kubwa yenye mwangwi…” Mfalme Zumaridi alisimulia maajabu.

Baada ya mazungumzo hayo na ‘Mungu’ wake, Mfalme Zumaridi anasimulia kwamba aliamrishwa kunyanyuka kutoka kitandani na kupanda kwenye mgongo wa simba na baada ya sekunde kadhaa akajikuta kuzimu wametua.

Kipindi ananyanyuka, aliamrishwa kuangalia alichokiacha nyuma na kuona ni mwili wake, na kuambiwa kwamba huo ndio mwili unaobaki mtu anapokufa na alichokwenda nacho ni roho tu.

“Kule kuzimu tukawa tunatembea, ninaoneshwa watu waliokufa, ni mifupa tu. Kule kuzimu kulikuwa na giza kubwa lakini tulipofika mwanga ukatokea mkubwa ajabu. Cha ajabu nilichokiona kule kuzimu, wale watu wananifuata mimi kama kwamba mimi ndio mkombozi wao….” Bundala alisimulia, akisema alikuwa anaongozwa na Simba yule ambaye alikuwa ni ‘Mungu’.

Baada ya hapo, waliondoka na yule Simba na mara ghafla akarudishwa nyumbani alikokuwa amelala na mama yake.

Mchungaji huyo wa ajabu ambaye juzi amefutiwa mashtaka alisema kwamba baadae alipoolewa alipata wokovu na nguvu mpya kiasi kwamba alikuwa akianza maombi, yanadumu kwa saa 9 mfululizo akiwa ameinua mikono juu.

“Mume wangu akaja akaniacha na nikarudi nyumbani nikajiwa na maono nikajikuta katika uflame wa Mungu, mbunguni kabisa. Baadae akaja malaika kunichukua katika ofisi ya Mungu Baba. Ule mwanga ulionitoa duniani ukanikaribisha. Mungu akaniambia kwamba amenileta Mbinguni kwa agano la kuiongoza dunia. Nikachukua kalamu ya chuma kama dhahabu na nikaweka saini.”

“Yesi mimi nimeshamuona mara nyingi, mbinguni nimeenda mara nyingi tu. Mbinguni nyumba ni ndefu maghorofa, minara mirefu halafu yote ni ya dhahabu. Watu wote wanafanana na sura moja tu. Wote wanafanana kama Wachina,” Mfalme huyo alisema.