RIP: Afrika Kusini yapoteza msanii mwingine wa tatu ndani ya wiki tano

Gloria Bosman amefariki siku chache tu baada ya kifo cha Costa Titch aliyepoteza fahamu jukwaani, mwezi mmoja baada ya kifo cha AKA.

Muhtasari

• Mwanamuziki huyo hivi majuzi aliteuliwa katika bodi ya Samro (shirikisho la hakimiliki za wasanii wa Afrika Kusini) kama mkurugenzi asiye mtendaji.

• Hata hivyo, Samro hawakuweka wazi kiini cha kifo cha malikia huyo wa Jazz.

Gloria Bosman, msanii wa Jazz aliyefariki.
Gloria Bosman, msanii wa Jazz aliyefariki.
Image: Instagram

Kwa mara nyingine tena, taifa la Afrika Kusini limetupwa kwelie kipindi cha maombolezo. Hii ni baada ya taarifa za kifo cha msanii mwingine, Gloria Bosman, aliyekuwa msanii wa Jazz.

Gloria Bosman, alifariki akiwa na umri wa miaka 50 na taarifa zake kulingana na jarida la Soweto, zilifichuliwa na shirikisho la hakimiliki za kkazi za Sanaa za wasanii wa taifa hilo lenye raia wenye rangi ya ngozi ainati.

Mwanamuziki huyo hivi majuzi aliteuliwa katika bodi ya Samro (shirikisho la hakimiliki za wasanii wa Afrika Kusini) kama mkurugenzi asiye mtendaji.

Bosman alizaliwa Mofolo katikati mwa Johannesburg na kukulia Pimville, Soweto. Anajivunia Tuzo mbili za Muziki za Afrika Kusini (Samas) na uteuzi zaidi ya 11, pamoja na uteuzi wa Kora mara mbili, Soweto Live waliripoti.

Albamu ya kwanza ya Bosman, Tranquility, ambayo ilitolewa katika miaka ya 1990, ilimletea tuzo ya heshima ya Mgeni Bora na kupokea uteuzi wa Albamu Bora ya Kisasa ya Jazz na Msanii Bora wa Kike katika Samas za 2001.

 

Kifo cha msanii huyo maarufu wa Jazz kinakuja siku chache tu baada ya kifo cha msanii wa Amapiano, Costa Titch kuzuka.

Titch, bingwa wa Amapiano alifariki baada ya kudondoka jukwaani alikokuwa akitumbuiza, kulingana na mikanda ya video ambayo imekuwa ikisambazwa na kuenezwa mitandaoni.

Vifo vya wawili hawa vinakuja chini ya wiki tano tu baada ya kifo cha ghafla mno cha msanii AKA ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana ambao walimvizia kwenye mmgahawa mmoja nchini humo.