Msanii wa Afrobeats kutoka Nigeria, Davido, kwa mara nyingine tena amekuwa gumzo la mitandaoni baada ya kufuta picha zote kwenye ukurasa wake wa Instagram na kubakisha machapisho 3 tu!
Davido ambaye amekuwa mwenye kimya kirefu tangu Novemba mwaka jana alipompoteza mwanawe wa pekee Ifeanyi amekuwa akipitia wakati mgumu sana wa kukubali kifo hicho, kulingana na wandani wake.
Msanii huyo siku tatu zilizopita alifanya kitendo kinachotafsiriwa na wengi kuwa huenda bado anaumia kutokana na kifo cha mtoto wake, baada ya kufuta picha zote ikiwemo ile ya utambulisho kwenye jalada la Instagram.
Machapisho matatu ambayo aliyabakisha ni lile la picha ya mtoto wake marehemu ambayo alipakia kumsherehekea siku yake ya kuzaliwa siku chache kabla hajafa, ya pili ikiwa ni ya pamoja akiwa na mkewe Chioma jukwaani na chapisho la tatu likiwa la picha ambazo alipigwa akitumbuiza jukwaani katika hafla ya kufunga mashindano ya kombe la dunia Qatar mwezi Desemba.
Wafuatiliaji wake walilitafsiri tukio hilo kwa njia tofauti, wengi wakionekana kukubali kwamba picha hizo tatu alizoziacha zina upekee katika maisha yake na ambazo zote zina maudhui yanayozuguka kifo cha mwanawe kwa njia moja au nyingine.
Katika picha ya kwanza ambayo ni ya Ifeanyi, baadhi walihisi kwamba Davido aliiacha ili kuendelea kusalia kama kumbukumbu ya aliyekuwa mrithi wake wa kipekee.
Picha ya pili ambayo wanaonekana na mke wake Chioma ilichambuliwa kuwa ina upekee kwani ndiye mwanamke aliyemzalia mtoto aliyekuwa anampenda sana kama mrithi wake kabla ya umauti kumnyakua.
Picha ya tatu akiwa jukwaani Qatar pia ilitajwa kuwa na kumbukumbu za kipekee kwani huo ndio wakati alionekana kwa mara ya kwanza hadharani baada ya kifo cha mtoto wake kilichomtupa gizani kwa takribani mwezi mmoja.
Hata hivyo kabla ya kufanya kitendo hicho, Davido mapema wiki jana aliandika kwenye Instastory yake kwamba mwezi huu wa Machi angerudi kwenye muziki kwa kishindo, akidokeza kuwa ana albamu mpya atadondosha baada ya kimya cha muda wa miezi takribani 6.