Wahu apaza sauti kuhusu kifo cha msichana aliyefariki darasani akifanya mtihani

Msichana huyo alikuwa mgonjwa, akaenda kliniki ya shule kutafuta matibabu lakini akafurushwa akitakiwa kurudi darasani ili kumaliza mtihani, alifariki akifanya mtihani.

Muhtasari

• Wahu alisema kuwa ulikuwa ni utepetevu wa kiwango cha juu kutoka kwa uongozi wa shule ambao haukutaka kumsikiliza msichana huyo.

koki, msichana aliyefariki darasani.
koki, msichana aliyefariki darasani.
Image: Facebook

Wiki iliyopita shule ya wasichana ya Njoro iligonga vichwa vya habari ikisutwa kwamba ilitepetea katika jukumu lao kama walimu mpaka kupelekea kifo cha msichana mmoja aliyetambulika kama Koki.

Msichana huyo aliyefariki alisemekana kuwa alikwenda katika ofisi akiripoti kwamba alikuwa anahisi kuwa mgonjwa lakini badala ya kupewa huduma ya matibabu, alirudishwa darasani akitakiwa kulamiza mtihani wa nusu muhula, lakini kwa bahati mbaya alifariki katikati ya mtihani huo.

Watu mbalimbali mitandaoni waliisuta shule hiyo na mwanamuziki Wahu amekuwa mtu wa hivi karibuni kukashifu kitendo cha shule hiyo kumnyima mwanafunzi haki ya matibabu hadi kufariki darasani.

Wahu, ambaye ni mama wa mabinti watatu alisema kwamba si vizuri kwa uongozi wa shule kupania mwanafunzi kufanya mtihani wakati anasema kuwa ajihisi vizuri katika afya ya mwili, kwani kunao maisha baada ya mitihani.

“Nimesoma hadithi hii ya kuhuzunisha sana. Mwanafunzi akilalamika kuwa hajisikii vizuri, ana joto kali na ukamfanya akae mitihani yake, huo ni uzembe wa hali ya juu. Mama Koki....na familia ya Koki Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu.🙏🏾💔” Wahu aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Kulingana na Mama Koki, muuguzi katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Njoro alimfukuza kijana huyo ambaye alikuwa mgonjwa licha ya kwenda kliniki akiungwa mkono na wanafunzi wenzake.

Msichana shupavu, ambaye alikuwa akiendelea kumwambia mwalimu hajisikii vizuri lakini akaambiwa amalize mitihani, akarudi darasani na kuketi kwa karatasi yake ya Kemia ambapo umauti ulimpata.