Je, ni kweli kwamba mchekeshaji Mulamwah na mrembo Ruth K ni wapenzi wa kisiri au ni urafiki tu?
Ndilo swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza na litabaki kuwa swali gumu kwa muda, kwani wengi wanahisi ukaribu wao wa kuitana ‘Bestie’ ni Zaidi ya urafiki.
Hata hivyo, wawili hao wamekuwa wakisisitiza kwamba hakuna kinachoendelea kati yao Zaidi ya urafiki wa kawaida tu – yaani bestie.
Wawili hao kwa mara nyingine tena wameibua ukakasi mtanange kwenye ukurasa wa Facebook, baada ya Mulamwah kupakia video wakiwa na Ruth K.
Walikuwa wakitembea wakitoka nje ya jumba la kifahari ambapo Mulamwah alifichua kwamba walikuwa wanatoka kuishtaki njaa katika mgahawa ulioko ndani ya jumba hilo la kibiashara mjini.
Mulamwah alisema kwamba mpenzi wake ndiye safari hii aligharamia chakula cha mchana.
Baada ya kutembea kwa muda wakiwa wanatabasamiana kwa furaha, Ruth K alisimama mbele ya Mulamwah na kumkaribia kama mtu anayetaka kumpa busu midomoni.
Hata hivyo, Mulamwah alimkaribia pia kabla ya wawili hao kukumbatiana kwa mahaba mazito ila Mulamwah akatoa tahadhari kwa wanamitandao kutofikiria kwamba wangeenda pamoja.
“Bestie leo amenunua chakula cha mchana… raundi kiasi mjini halafu kila mtu aende kwake,” Mulamwah alisema.
Ruth K kwa upande wake alipakia video hiyo na kuinukuu kwa maneno, "Nikifurahia chakula cha mchana na bestie"
Itakumbukwa mwaka 2021 mara baada ya kutangaza kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonie, Mulamwah alidakia mitandaoni na kupakia picha na video wakiwa pamoja na Ruth K, jambo lililowaaminisha wengi katika falsafa ya “kuoga na kurudi soko” pasi na kusubiri muda vumbi kutulia.
Kwa muda, Mulamwah alijulikana kutoka kimapenzi na mrembo huyo hadi pale alipofanya mahojiano akisema kwamba hajakuwa na mpenzi tangu kuachana na mama wa mtoto wake, akimtaja Ruth K kama rafiki tu – hata hivyo wengi hawajaonekana kuamini na usemi huu wake – kwa jinsi wanaonekana pamoja katika mazingira ya kudokeza uwezekano wa mahaba.