Wanahabari wa Kiswahili katika runinga ya NTV, Lofty Matambo na Fridah Mwaka ambao mara nyingi huitana hewani kama ‘pacha wangu’ kwa mara ya kwanza wamezungumzia uhusiano wao.
Wawili hao ambao walikuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kushuhudia shoo kubwa ya ucheshi ya mchekeshaji MCA Tricky kwa jina ‘Tricky Comedy Circuit’ walinyoosha maelezo kuhusu dhana vichwani mwa watazamaji wa runinga kuwa wao ni wapenzi.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwao kuweka wazi kama ni kweli wao ni wapenzi au la, lakini kwa namna moja au nyingine, walipuuzilia mbali dhana hiyo wakiwataka wambea wanaolenga kuchokonoa ukweli kuhusu uhusiano wao “kufagia kwao” kwanza.
“Ukaribu wenu nyinyi wawili kuna vile watu wanasema mwapendeza hadi wengine wanashuku kwamba mko kwenye mahusiano ya kimapenzi hivi, ni kweli?” mwanablogu mmoja aliwasakama kooni.
Matambo alilikwepa swali hilo akilielekeza kwa Mwaka ambaye alijibu akisema;
“Lakini mimi nko na swali kwenu, kuna shida gani tukiwa na ukaribu, nyinyi wenyewe mwafurahishwa na ukaribu wetu. Fagieni kwenu!” Fridah Mwaka alijibu huku wakiguna kwa zamu na Matambo baina ya vicheko.
Matambo alifunguka kwa nini aliamua kuhudhuria katika hafla ya Tricky na ukaribu wao upoje ambapo alisema walijuana enzi hizo wakifanya kazi katika kituo kimoja cha redio, zamu tofauti.
Wawili hao japo walitokea na mavazi ya Kiislamu, walikanusha kuwa wao si Waislamu bali ni Wakristo lakini wakasema kuvalia vile ni kuonesha kwamba wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadan na marafiki, mashabiki na wafanyikazi wenzao ambao wamefunga katika mwezi mtukufu.
Ukaribu wa wawili hao umekuwa ukilinganishwa na ule wa wanandoa Rashid Abdalla na Lulu Hassan ambao pia hufanya kipindi kimoja cha habari za kiswahili katika runinga ya Citizen.